GAZETI LA MSETO LAPEWA SIKU 7 KUMWOMBA RADHI NAIBU WAZIRI WA UJENZI MHE. NGONYANI
Naibu Waziri wa Ujenzi,
Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi. Edwin A. Ngonya
******************************
Naibu Waziri wa Ujenzi,
Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi. Edwin A. Ngonyani amelitaka gazeti la Mseto
kumuomba radhi na kumlipa fidia ya shilingi bilioni moja kutokana na kuandika
habari ya kumchafua.
Akizungumza na waandishi
wa habari Ofisi kwake Waziri Ngonyani amesema kuwa Gazeti hilo la tarehe 4
Agosti 2016 liliandika habari yenye kichwa cha Habari “Waziri amchafua JPM”
ikimuhusisha na upokeaji wa fedha kutoka moja ya Kampuni ya Madini wakati akiwa
Kaimu Mkurugenzi wa Shirika la Madini la Taifa (Stamico).
“Nimewaandikia notisi ya
siku saba ikiwataka waombe radhi na kunilipa fidia, na wasipofanya hivyo hatua
stahiki kuwapeleka mahakamani akiwemo Mwandishi Josephat Isango, Mwanahalishi
Publisher na Mchapaji wa gazeti hilo”. Alisema Mhandisi Ngonyani.
Mhandisi Ngonyani
amesema kuwa habari hiyo siyo ya kweli na mwandishi ametumia nyaraka za
kughushi ikiwemo barua iliyoandikwa tarehe 24 Julai na kutiwa saini yake akiwa Kaimu Mkurugenzi
wa STAMICO wakati ukweli ni kwamba tarehe hiyo yeye alikuwa ni Mkurugenzi
kamili na siyo Kaimu kama barua hiyo inavyosomeka.
Ameongeza kuwa habari
hiyo imewachafua watu wengi ikiwemo familia yake, wapiga kura wake wa jimbo la
Namtumbo ambao walijitoa katika kumsaidia wakati wa kampeni na hali kadhalika
zimemchafua Mhe. Rais Dkt. John Pombe Magufuli kwa kumhusisha na fedha kutoka
kwa wawekezaji wa nje kwa kuwaahidi kuwa mitaji yao nchini itakuwa salama.
“Mheshimiwa Rais Dkt.
Magufuli alishasema kama kuna mfanyabiashara yeyote aliyechangia kuingia kwake
ikulu ajitokeze na hakuna aliyefanya hivyo, Iweje leo mtu tu anaibuka na
kuandika habari za kugushi? ”. Aliongeza.
Aidha Naibu Waziri huyo
ametumia fursa hiyo kuwataka waandishi wa habari nchini kuwa waangalifu pindi
wanapoandika habari za kutunga kwa kutotumia majina halisi kwani kufanya hivyo
ni kwenda kinyume na kanuni za uandishi wa hadithi (Habari za kutunga).
“Waandishi wa habari
mnatakiwa kufuata maadili ya kazi yenu kwa kuandika habari zenye ukweli ili
kuliepusha taifa kuingia katika machafuko na
migogoro isiyo ya lazima” Alisema Naibu waziri huyo.




