KUTOKA IRINGA; CHUI AIBUKA NA KUPOTEA HOSPITALI YA MKOA
AMA
kweli ukistaajabu ya musa utayaona ya firauni.... Katika hali
isiyotarajiwa chui wa ajabu amezua
taharuki kubwa kwa wagonjwa na wauguzi katika Hospitali ya Rufaa ya mkoa wa
Iringa baada ya mnyama huyo kuibuka katika mazingira ya kutatanisha.
Akizungumzia
juu ya tukio hilo muunguzi mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya mkoa wa Iringa
Rustica Tung’ombe alisema tukio hilo
limetokea majira ya saa 7 na saa 8 usiku wa kuamkia leo Jumatano na kwamba chui
huyu alionekana nje eneo la wodi namba 6 .
Alisema
kw mujibu wa taarifa zilizoripotiwa na muuguzi msimamizi wa zamu usiku ni
kwamba wanawake ambao walikuwa wakitoka kunyonyesha watoto wao wodini
walikimbia huku wakipiga kelele za kuomba msaada baada ya kukutana na chui
huyo.
"Kulikuwa
na kundi la kwanza la akina mama waliotoka kunyonyesha watoto wao lilipita eneo
hilo na kundi la pili lilifuata na mwanamke mmoja kati yao alikuwa nyuma
akifuata wenzake na ndipo alipomshuhudia chui huyo na kuanza kupiga kelele
……wauguzi walipochungulia madirishani walipata uhakika kuwa mnyama huyo ni chui
", alisema.
Kutokana
na kuwa na uhakika juu ya mnyama huyo kuwa ni chui walilazimika kuomba msaada
kwa askari magereza ambao wamepakana na hospitali hiyo kwa ajili ya kutoa
msaada.
Alisema
baada ya kufika askari magereza pamoja na kundi kubwa la wananchi kwa ajili ya
kupambana na chui huyo ghafla mbwa aliibuka nyuma ya chui huyo na kuanza
kumfukuza chui huyo ambaye aliruka ukuta wa uzio na kutoweka kusikojulikana.
“Wakati
askari magereza wanajiandaa kupambana na chui huyo alitokea mbwa ambaye kweli
hatujui alitokea wapi na kuanza kumfuatilia chui huyo ….. hili ni tukio la aina
yake na halijapata kutokea katika Hospitali hii maana hapa ni mjini na hatujui
chui huyu kafikaje hapa”
Na
MatukiodaimaBlog




