Wanafunzi Wazimia Na Kupoteza Fahamu Baada Ya Kumuona Akwilina Ndani Ya Jeneza

Vilio, simanzi na
kupoteza fahamu kwa baadhi ya wanafunzi ni baadhi ya matukio ya huzuni
yanayojitokeza katika Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT), baada ya kuwasili
mwili wa aliyekuwa mwanafunzi wa chuo hicho, Akwilina Akwiline.
Mwili wa mwanafunzi huyo unaagwa leo,
Februari 22, 2018 katika viwanja vya chuo hicho.
Wanafunzi zaidi ya
wanne aliokuwa akisoma nao Akwilina chuoni hapo ni kama hawaamini baada ya
kushuhudia jeneza lenye mwili wake, huku wengine wakipoteza fahamu na kupewa
huduma ya kwanza na Shirika la Msalaba Mwekundu.
Viongozi waliofika
mpaka sasa katika viwanja vya NIT ni Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga
Taifa, Dk Hussein Mwinyi; Waziri wa Elimu, Profesa Joyce Ndalichako; Naibu
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Hamad Masauni; Kamanda wa Polisi Kanda
Maalumu ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa na Mbunge wa Kibamba (Chadema), John
Mnyika.
Tayari ibada ya
kuaga mwili wa mwanafunzi huyo imeanza.





