Breaking News

GST YASISITIZA TAFITI ZA MADINI KUONGEZEA MIGODI NA VIWANDA ENDELEVU

Na Mwandishi Wetu - Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST) imesisitiza umuhimu wa kuongeza shughuli za utafiti wa madini nchini ili kugundua maeneo mapya yenye viashiria vya madini, kuongeza migodi na kuhakikisha upatikanaji wa malighafi za uhakika kwa ajili ya viwanda.

Mtendaji Mkuu wa GST, Ali Samaje, amesema taasisi hiyo ina jukumu la kukusanya na kutoa taarifa za kisayansi zinazohusu jiolojia, jiokemia na jiofizikia ili kuwaongoza watafiti na wawekezaji kutambua maeneo yenye viashiria vya madini na hivyo kurahisisha shughuli za utafiti.

Amesema upatikanaji wa taarifa hizo unasaidia kupunguza gharama za utafiti, muda na changamoto zinazoweza kujitokeza kwa wawekezaji wanapotafuta maeneo yenye madini, kwa kuwa wanaweza kuelekezwa moja kwa moja katika maeneo yenye viashiria vya uwepo wa rasilimali hizo.

Akizungumza katika mdahalo wa kuhamasisha uwekezaji katika sekta ya madini, Samaje amesema GST inaendelea kutekeleza jukumu lake la kuhakikisha taarifa za kisayansi zinapatikana na kutumiwa kuongeza ufanisi katika shughuli za utafiti na ugunduzi wa mashapo mapya ya madini.

Amesema sekta ya madini ni miongoni mwa sekta muhimu katika kukuza uchumi wa taifa na kuchangia utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, hivyo kuna umuhimu wa kuongeza thamani ya madini kwa kuwekeza katika viwanda vya kuchakata, kuyeyusha na kusafisha madini, pamoja na viwanda vinavyotumia madini kama malighafi kuzalisha bidhaa za mwisho.

Ameeleza kuwa kufikia hatua hiyo kunahitaji kuwepo kwa hazina ya uhakika ya madini, jambo ambalo linawezekana kupitia kuimarisha na kuongeza shughuli za utafiti ili kugundua maeneo mapya yenye rasilimali hizo na kuanzisha migodi zaidi.

Samaje amesema GST ina nafasi muhimu katika kuhakikisha sekta ya madini inakuwa msingi wa maendeleo ya viwanda nchini kwa kutoa taarifa zinazowezesha ugunduzi wa mashapo mapya na kuongeza upatikanaji wa madini yatakayotumika kama malighafi katika uzalishaji wa bidhaa mbalimbali.

Amesisitiza kuwa uwepo wa taarifa sahihi za jiosayansi na kuongezeka kwa shughuli za utafiti ni msingi wa kuwa na uzalishaji endelevu wa madini na kuhakikisha viwanda vinapata malighafi za kutosha kwa muda mrefu.