Utitiri Wa Makanisa Wamshtua Rais

Wakati
Bodi ya Utawala Bora nchini Rwanda (RGB) ikisitisha shughuli za makanisa 714 na
msikiti mmoja, kwa kushindwa kufikia vigezo vinavyotakiwa katika kuendesha
shughuli zao, Rais Paul Kagame ameelezea kushitushwa na idadi hiyo kubwa ya
makanisa nchini mwake.
Rwanda,
taifa la Afrika Mashariki lenye wakazi 11,262,564, kwa mujibu wa Sensa ya mwaka
2012, wakazi wake wengi ni Wakristo, hasa Waprotestanti ambao ni asilimia 49.5,
Wakatoliki asilimia 43.7 na Waislamu ni asilimia mbili. “Makanisa 700 ndani ya
Kigali? Hivi ni visima vinavyowapa watu maji?” alihoji Rais Kagame baada ya
kusikia hatua zilizochukuliwa dhidi ya makanisa hayo.
“Sina
visima vingi kiasi hiki. Pia tuna idadi kubwa ya viwanda? Lakini makanisa 700,
ambayo pia mengine yanafungwa? Hakika inashangaza sana!” Rais Kagame aliyasema
hayo hivi karibuni wakati akifunga `semina elekezi’ ya siku nne kwa viongozi wa
umma nchini Rwanda. Alisema kwa uelewa na imani yake, Rwanda haijafikia hatua
ya kuhitaji idadi kubwa ya makanisa kama inayosikika.
“Kama
taratibu zingekuwa zinafuatwa, tusingefikia hatua hii ya kufungia makanisa.
Lakini kwa hatua hii, sitashangaa kuona hatua ya Serikali ikipigiwa kelele kuwa
ni ukiukwaji wa haki za binadamu. Najua watu wana haki za kuabudu, lakini
taratibu lazima zifuatwe,” alisema Rais Kagame.
Vigezo
vilivyotumika kufungua makanisa na msikiti mmoja, vimetajwa kuwa ni pamoja na
kutodhibiti kelele, usafi duni na pia mazingira yasiyo salama kwa waumini wao.
“Baadhi ya makanisa yanaendesha ibada katika mazingira hatarishi na yasiyo masafi,
kiasi cha kutishia afya na usalama wa watu,” anasema Anastase Shyaka, Mkuu wa
RGB inayosimamia taasisi za umma na binafsi nchini Rwanda. “Suala la kelele pia
limeripotiwa, hili limekuwa sugu kwa baadhi ya makanisa. Ndiyo maana tumeamua
kuchukua hatua.
Hatutayaruhusu
kufanya kazi hadi hapo yatakaporekebisha dosari,” alisisitiza Shyaka.



