Askofu GWAJIMA Aanza Kuliamsha Dude....Asimulia Kisa Cha Mwanamke

Askofu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima,
Josephat Gwajima ameeleza namna alivyonyang’anywa samani na muumini wake siku
chache baada ya kumkabidhi.
Akitoa mahubiri katika ibada jana
Aprili 15,2018 kanisani kwake, Ubungo jijini Dar es Salaam, Askofu Gwajima
alisema aliamua kumrudishia muumini huyo na kukubali kuaibika.
Akisimulia kisa hicho mbele ya mamia
ya waumini, Askofu Gwajima alisema wakati anaanza maisha na kazi ya kuendesha
kanisa hilo, alipanga chumba kimoja katika eneo la Ubungo Msewe.
“Katika chumba nilichokuwa nimepanga
kitu cha thamani nilichokuwa nacho ilikuwa ni carpet (zuria) la plastiki,”
alisema.
Alisema wakati akiendelea kuishi
katika chumba hicho, alitembelewa na muumini wake aliyemtaja kwa jina moja la
Ester.
“Ester baada ya kuona mazingira ya
chumba kile, akaniambia mchungaji hapa panahitajika stuli kwa ajili ya kukalia,
nitazileta,” alisema.
Askofu Gwajima alisema kweli muumini
huyo alimpelekea stuli nne na yeye akamshukuru kwa msaada huo.
“Baadaye muumini huyo akawa anatamba
kanisani akiwaeleza waumini wenzake kwamba stuli zilizoko kwa mchungaji
zimepelekwa na yeye,” alisema.
Gwajima alisema muumini huyo akawa
anataka waumini wenzake wathamini mchango ambao anautoa kwa mchungaji.
“Baada ya kusikia hilo tulimwita na
kumuonya asiwatishe waumini kwa kutumia kigezo cha msaada huo,” alisema.
Aliongeza, “siku moja nilitembelewa
na ndugu zangu akiwemo mjomba, wakakaa kwenye stuli zile. baada ya muda mfupi
Ester akaingia na kudai stuli zake mbele ya ndugu zangu.”
“Nikamtoa nje ili tuzungumze lakini
msimamo wake ukawa uleule apewe stuli zake, ndugu zangu wakawa wanashangaa
hawaamini kinachotokea,” alisema.
“Mjomba wangu akanieleza kwamba ina
maana Gwajima huna hata stuli kwenye chumba chako.
“Nikamwambia stuli hizo si mali yangu
ni za muumini hivyo nikawataka wageni wale wakae kwenye zuria, nikampa stuli
zake.”
Amewataka waumini hao wasiogope
kuaibishwa na mtu kwa sababu hatima ya maisha yao ipo palepale.
“Ni kweli niliaibishwa mbele ya ndugu
zangu lakini sikukata tamaa na hatima ya maisha yangu ilikuwa palepale kama
mnavyoniona leo,” alisema.



