Breaking News

Mbatia: Vyama Vya Siasa Vijenge Misingi Bora Ya Uongozi Kwa Faida Ya Vizazi Vilivyopo Na Vijavyo Pamoja Na Ustawi Wa Taifa.

Na Hussein Ndubikile, Dar es Salaam

Vyama vya Siasa nchini vimeshauriwa kujenga misingi bora ya uongozi itakayosaidia kujenga viongozi bora wa vizazi vilivyopo na vijavyo pamoja na ustawi wa taifa.

Hayo yamesemwa leo jijini Dar es Salaam na Mwenyekiti wa Taifa wa Chama cha NCCR MAGEUZI, James Mbatia katika Mkutano Mkuu wa chama hicho wenye lengo la kupata Wagombea Urais wa Tanzania Bara na Zanzibar.

Alisema kuwa vyama vyote vya siasa vina jukumu kutengeneza mifumo thabiti ya kiuongozi itakayoimarisha jamii hasahasa vijana wanaoingia kwenye nafasi za uongozi.

“ Tuweke misingi na mifumo bora ya uongozi itakayosaidia vizazi vilivyopo na vinavyokuja ujengaji huu utasaidia kuimarisha ustawi wa amani ya taifa,” alisema Mbatia.

Alibainisha kuwa viongozi bora hawapatikani katika misingi ya siasa isiyo imara na badala yake hujengwa kwenye mifumo sahihi ya kiuongozi.

Alisisitiza kuwa chama hicho katika kampeni za uchaguzi mkuu kitaendelea kukazia misingi ya Katiba, uimarishaji uchumi kwa vitendo pamoja na kuboresha mfumo wa elimu ili uwakomboe vijana.

Alifafanua kuwa wagombea wa chama wajipange kutumia ndimi zao vyema ili waweze kupata nafasi za ubunge, udiwani na urais na kubainisha kuwa vyombo vya dola visitumia nguvu kubughudhi watu wakati wa uchaguzi.

Aliwashukuru wabunge waliofanikisha kufanyika kwa mkutano huo kwa kuchangia michango yao akiwemo Anthony Komu, Suzan Masele pamoja na Joseph Selasisni.

Mgeni Mualikwa wa mkutano ambaye pia ni Mkurugenzi wa Taasisi ya Mwalimu Nyerere, Joseph Butiku aliwasihi kukijenga chama kisicho tama ya mali na madaraka ya kutawala wengine bila ridhaa yao.

Naye Msajili Msaidizi wa Vyama vya Siasa Sisty Nyahoza alivisiasa vyama vya siasa kufanya siasa za kistaarabu na kuacha propaganda za uongo  kuwa Ofisi ya Msajili wa vyama hivyo inapendelea chama kimoja.