Vyombo Vya Habari Vimetakiwa Kuripoti Taarifa Sahihi za Kitafiti Nchini
Mhariri Mkuu Msaidizi wa Jarida la Afya ya Jamii Tanzania (The Tanzania Public Health Bulletin) akiwasilisha mada katika mafunzo kuwajengea uwezo Wanahabari (hawapo pichani) yaliyofanyika jijini Dar es salaam.
Mhariri Mkuu Msaidizi wa Jarida la Afya ya Jamii Tanzania (The Tanzania Public Health Bulletin) akimkabidhi kijarida kwa moja washiriki mafunzo ya siku mbili kwa mwandishi wa gazeti la the Citizen bw. John Namkwahe jijini Dar es salaam.
Na Mwandishi Wetu.
VYOMBO vya Habari na Waandishi wa Habari nchini wametakiwa kuripoti taarifa sahihi za wataalam wa afya wakiwemo watafiti mbalimbali kwa lengo la kuondoa hofu na mtafaruku kwa Jamii.
Hayo yamesemwa Jijini Dar es Salaam na Mhariri Mkuu Msaidizi Dk. Julius Massaga wakati akielezea Jarida maalum la Afya ya Jamii Tanzania (The Tanzania Public Health Bulletin) ambalo linachapisha habari mbalimbali za kitafiti kwa lugha rahisi na nyepesi inayoweza kueleweka kwa wote hata wale ambao siyo wataalamu wa afya.
Alisema, semina hiyo ilikuwa na lengo la kuwapiga msasa Waandishi wa habari kuweza kuandika habari kwa weredi zaidi pamoja na kulitamburisha jarida hilo.
"Lengo kuu ya semina hii ni kuwataarifu kuhusu Jarida letu la Jamii. Lakini pia kukumbushana umuhimu wa kuandika habari ambazo zinatoka vyanzo vya kuaminika na habari zenyewe ziwe na uhakika na kwamba ziwe na ukweli (evidence-based) na sio tu mtu anachukua kutoka vyanzo vyake ambavyo haviaminiki" alisema Dk. Massaga.
Akielezea suala la hofu kutokana na habari zisizofuata misingi alibainisha:
"Wanahabari wanapoandika habari waandike za kweli na zisizoleta mshtuko kwa watu ama taarifa zenye kuleta hofu kwa watu kama tulivyoona katika ugonjwa wa COVID 19.
Baadhi ya taarifa zilizokuwa zinatoka wakati wa COVID 19 ambazo zingine zilikuwa zinawatia hofu wananchi.
Kwa hiyo tulikuwa tunawataarifu kwamba taarifa lazima ziandikwe zisilete hofu, isopokuwa zitoe taarifa ambazo zitawasaidia wananchi kuelewa tatizo na kuweza kujikinga ama kutafuta namna ya tiba ya kuweza kujitibu." Alisema Dk. Massaga
Dk. Massaga alibainisha kuwa, Washiriki wameweza kupata muktadha wa malengo ya jarida hilo lakini pia kupata yale yanayofaa kwa kuweza kuwakumbushia Uandishi ulio wa nadhifu kwa taarifa zitoke na kuwafikia wananchi kama walaji na watumiaji kwa minajiri ya kuwasaidia na si kuwatia hofu.
Aidha, ameeleza kuwa, mpaka sasa wameshatoa majarida manne.
Miongoni ni pamoja na taarifa kuhusu mlipuko wa ugonjwa wa Dengue, lakini pia wametoa jarida lenye makala kuhusu namna ya kuzuia kichaa cha mbwa ikiwemo kuchanja mbwa wenyewe.
"Mpaka sasa tumeshatoa majarida manne.
Baadhi ya majarida hayo ni pamoja na toleo lenye makala maalum linalo husu mlipuko wa Dengue. Lakini pia tuna toleo ambalo ni 'policy brief' kuhusiana na namna gani ya kukabiriana na kichaa cha mbwa ikiwemo kuelezea namna ya kuwachanja mbwa wenyewe" Alisema Dk. Massaga
Jarida hilo la Jamii Tanzania ni la Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii Jinsia, Wazee na Watoto ambalo lipo chini ya Mganga Mkuu wa Serikali, ambaye ndiyo Mhariri Mkuu. Jarida hilo limeanzishwa kwa ajiri ya kutoa taarifa za kina za Wizara na Kitafiti ambazo zina manufaa kwa jamii.
"Jarida limeanzishwa kwa minajiri ya kutoa taarifa za Wizara ya Afya kwa Wananchi kwa sababu ilionekana kuna taarifa ambazo zingine zinazalishwa katika wizara ya afya lakini haziwafikii wananchi na Wanahabari ilikuweza kufanyiwa kazi" Alisema Dk. Massaga.
Tokea kuzinduliwa kwa jarida hilo Juni 2019, hadi sasa tayari wamesha chapisha na kutoa majarida manne (4), ambapo majarida hayo hutolewa mara moja kila baada ya miezi mitatu.
Semina hiyo ya siku mbili kwa Wanahabari kuripoti Habari za afya kwa weredi, imeandaliwa na Wizara ya Afya kupitia jarida la Tanzania Public Health Bulletin (TPHB) kwa ufadhili wa shirika la Kimarekani la CDC Foundation.
Washiriki wa mafunzo hayo wakiwa katika Picha ya pamoja






