SHIBUDA: Vyama vya Siasa Tulinde Tunu za Taifa
Vyama vya siasa nchini vimetakiwa kulinda Tunu za Taifa za Utu, Ubinadamu, Amani na Utulivu, lugha ya kiswahili ya maneno ya hekma na busara kwa urithi wa vizazi vijavyo katika kipindi hiki cha uchaguzi.
Akizungumza Jijini Dar es Salaam na Mwenyekiti wa Baraza la Vyama vya Siasa Tanzania John Shibuda alisema wagombea wote wanatakiwa kunadi sera zao kwa hoja hili wapiga kura wafanye maamuzi yasiyoundwa na uongo wa siasa.
Aidha amewataka wagombea kuepuka kugeuza michakato ya kunadi siasa na sera kuwa mpango mkakati wa makusudi wa kughadhabishana wagombea na kuamsha mitazamo ya kufikirika kwamba kuna dhamira ya kificho ya kuvuruga umoja na undugu wa watanzania.
Sambamba na hayo amevitaka vyombo vya Dola kudumisha weledi na kuepuka kuchafulika na kuwa wahimilivu pale ndimi za wanasiasa zinapojikwaa na kunena maneno batili kwa sifa za uzalendo wa kutetea Taifa.
Hata hivyo ametoa wito kwa wapiga kura kujitokeza kusikiliza hoja za wagombea wote ili wapate uelewa wa kufahamu sifa zao na nani anafaa kuwa kiongozi wao ili siku ya kupiga kura wafanye maamuzi sahihi.
“Wapiga kura kumbukeni kwamba kila kura ni lindo la usalama na ni mtaji wa kunufaisha vizazi vyote hasa wasio na umri wa kupiga kura, kutokupiga kunaweza sababisha nchi kupata viongozi wasio waaminifu wa kutekeleza ndoto ya uhuru wa maendeleo kwa Jamii na Taifa” Amesema Shibuda.
Bw. Shibuda amesema siasa ovu na zana potofu huunguza amani, umoja na utaifa wa kuwa nchi ya jamii moja hivyo kuvunja amani ni rahisi ila ugumu ni kurejesha imani ya kujenga amani kati ya waliotenganishwa na imani hasi.




