TRA YAKUSANYA TRILIONI 16.9 JULAI 2021 HADI MACHI 2022
Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imesema kuwa katika kipindi cha robo tatu (3) yaani; mwezi Julai hadi Machi kwa mwaka wa fedha 2021/22 imekusanya Shilingi Trilioni 16.69 ikiwa ni sawa na ufanisi wa asilimia 97.3 ya lengo la kukusanya Shilingi Trilioni 17.15.
Makusanyo hayo ni ongezeko la Shilingi Trilionl 3.1 ukilinganisha na kiwango cha makusanyo cha Shilingi Trilioni 13.59 kilichokusanywa kwa kipindi kama hiki kwa mwaka wa fedha 2020/21. Ongezeko hili ni ukuaji wa makusanyo ya kodi wa asillmia 22.8.
Aidha kwa mwezi Machi 2022, TRA imekusanya Shilingi Trilioni 2.06 kati ya lengo la kukusanya Shilingi Trilioni 1.98. Makusanyo haya ni sawa na ufanisi wa asilimia 103.6 na ukuaji wa asilimia 23.17 ikilinganishwa na mwezi Machi 2021 ambapo makusanyo yalikuwa Shilingi Trilioni 1.67.
TRA imesema kuwa makusanyo haya kwa kiasi kikubwa yamechangiwa na kuongezeka kwa uhiari wa kulipa kodi, kuimarika kwa mahusiano baina ya TRA na walipakodi kunakochagizwa na utatuzi wa migogoro ya kodi nje ya mahakama pamoja na kushughulikia malalamiko ya walipakodi kwa wakati.
Pia , ufanisi huo umetokana na kuimarika kwa uzalishaji wa viwanda vya ndani na biashara za kimataifa.






