CUF YATANGAZA RASMI KUANZA MCHAKATO WA UCHAGUZI
CHAMA cha Wananchi (CUF) kimezindua rasmi shughuli za Uchaguzi Mkuu wa ndani ya Chama ambao utajumuisha na kuwapa fursa wanachama wote ya kuchagua au kuchaguliwa kuwa Viongozi katika ngazi mbalimbali ndani ya Chama.
Akizungumza makao makuu ya chama hicho buguruni jijini Dar es salaam Mkurugenzi wa Mipango na Uchaguzi wa CUF, Bw. Mwadini Jecha amesema Uchaguzi wa mwaka huu utakwenda sambamba na chaguzi za Jumuiya zote za Chama yaani Jumuiya ya Vijana (JUVI), Jumuiya ya Wanawake (JUKE), na Jumuiya ya Wazee yaani (JUZE).
“Chama kitangazia umma wa Watanzania hususan Wanachama, wapenzi na wale wanaokiunga mkono CUF-Chama cha Wananchi kwamba tunazindua rasmi leo shuguli za uchaguzi Mkuu wa ndani ya Chama,” Alisema Jecha
“Hivyo basi Wanachama wote wanapaswa kujipanga kuhakikisha kuwa wanashiriki kikamilifu katika kila hatua ya uchaguzi,”.
Jecha ametoa wito kwa Viongozi waliopo sasa na wanachama kwa ujumla kushuka chini kwenye ngazi ya matawi ili kuweza kujisajili upya kwa maana ya kufanya uhakiki wa uanachama wao kwa kila tawi na kufanya uhakiki wa matawi yatakayotimiza masharti ya Katiba ya Chama ya kuruhusiwa kufanya Uchaguzi kwenye matawi yao.
Amesema ni wajibu wa kila mwanachama kuhakikisha kuwa chama kinakuwa imara na chenye mvuto wa kisiasa kwa Wananchi.
“Hivyo ni muhimu kila mmoja wetu akashiriki kikamilifu kwenye kila hatua ya awali ya kufanya uhakiki wa matawi ili kufanikisha zoezi hilo la uchaguzi wa ndani ya Chama,” ameongeza Jecha.
Amewahimiza wanachama wenye nia ya kugombea nafasi mbalimbali za uongozi Ndani ya Chama katika uchaguzi huu, kwamba wenye nia ya kugombea nafasi za uongozi wa Kiserikali mwaka 2024 na 2025 waende kwenye matawi yaliyopo katika maeneo wanayoishi ili waweze kufanya uhakiki na kuahiriki kuhamasisha wanachama wengine ili kupatikana Viongozi makini.
Akizungumzia kuhusu ratiba ya uchaguzi huu amesema inaanza rasmi kesho Mei 14, 2022 na kukamilika Kati ya Septemba hadi Oktoba 2023.
Hivyo amewataka wanachama wenye sifa za kuwa Viongozi ndani ya Chama hicho wajitokeze kwa wingi kugombea nafasi mbalimbali kuanzia ngazi za chini hadi ngazi ya Taifa.




