Breaking News

ACT WAZALENDO: MARIDHIANO SI YA KUGAWANA MADARAKA, NI MSINGI WA MAGEUZI ZANZIBAR

Chama cha ACT Wazalendo kimesisitiza kuwa mchakato wa maridhiano ya kisiasa unaoendelea Zanzibar haukulenga kugawana madaraka au vyeo serikalini, bali kuweka msingi wa mageuzi ya kisiasa, kuimarisha demokrasia na kulinda haki za wananchi.

Akizungumza na waandishi wa habari, Makamu Mwenyekiti wa ACT Wazalendo Tanzania Bara, Isihaka Mchinjita, alisema msimamo wa chama hicho kuhusu Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK) haujabadilika tangu ulipoibuka mkwamo wa kisiasa baada ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015.

Alisema tangu mwanzo ACT Wazalendo ilieleza wazi kuwa haikuwa tayari kushiriki Serikali ya Umoja wa Kitaifa kwa lengo la kugawana madaraka au nafasi za uongozi, bali ilisimama kutetea mageuzi ya kisiasa yatakayorejesha heshima, haki na uhuru wa wananchi wa Zanzibar.

"Serikali ya Umoja wa Kitaifa si zawadi kwa vyama vya siasa wala fursa ya kugawana vyeo. Iliundwa kupitia marekebisho ya Katiba ya Zanzibar ya mwaka 2010 kwa lengo la kuwaleta pamoja Wazanzibari, kulinda amani, kuimarisha maridhiano ya kitaifa, kulinda haki ya wananchi kuchagua viongozi wao kwa uhuru na kuondoa ubaguzi wa kisiasa," alisema Mchinjita.

Alieleza kuwa mazungumzo yaliyodumu kwa takribani miezi minane chini ya usimamizi wa Marais wastaafu wa Zanzibar, Dkt. Amani Abeid Karume na Dkt. Ali Mohamed Shein, hayakujadili mgawanyo wa madaraka bali yalilenga kupata suluhisho la kudumu la migogoro ya kisiasa iliyoikumba Zanzibar kwa miaka mingi.

Mchinjita alisema historia ya Zanzibar imegubikwa na migogoro ya kisiasa tangu uchaguzi wa mwaka 1995, ikiwemo matukio ya vurugu na mauaji ya mwaka 2001 yaliyosababisha baadhi ya wananchi kukimbilia nchi jirani kama wakimbizi wa kisiasa.

Alidai kuwa matukio hayo yalionyesha umuhimu wa kujenga mfumo wa kisiasa unaohakikisha haki, amani na maridhiano ya kudumu kwa wananchi wa Zanzibar.

Kwa mujibu wa Mchinjita, ajenda kuu ya ACT Wazalendo katika mazungumzo hayo ilikuwa ni mageuzi ya kisiasa, si kushiriki Serikali ya Umoja wa Kitaifa.

Alisema kufikia Mei 2022, pande zote zilikuwa zimekamilisha majadiliano kuhusu ajenda muhimu za mageuzi na kukubaliana kuanza hatua ya kuandaa mfumo wa kisheria na kitaasisi wa kusimamia utekelezaji wa makubaliano hayo.
Alifafanua kuwa kushiriki hatua ya utekelezaji wa makubaliano hakumaanishi ACT Wazalendo imeingia serikalini, bali ni kuhitimisha hatua ya mazungumzo na kuanza kutekeleza makubaliano yaliyofikiwa.

"Iwapo utekelezaji wa makubaliano hayo utafikia hatua ambayo kwa mujibu wa sheria itahitaji kuundwa au kukamilishwa kwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa, suala hilo litashughulikiwa wakati wake," alisema.

Mchinjita alitoa wito kwa wadau wote wa siasa kuweka mbele maslahi ya Zanzibar, ustawi wa wananchi na mustakabali wa vizazi vijavyo badala ya maslahi ya muda mfupi, akisisitiza kuwa mafanikio ya mchakato huo yatategemea utekelezaji wa makubaliano kwa uaminifu na dhamira ya kweli kutoka kwa pande zote.