SAMIA KUZINDUA RIPOTI YA MIAKA 10 YA WATETEZI WA HAKI ZA BINADAMU NCHINI
Mratibu Kitaifa wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC), Onesmo Olengurumwa amesema kuwa Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan atazindua ripoti inayozungumzia hali ya watetezi wa haki za binadamu na asasi za kiraia nchini Tanzania kwa miaka 10.
Olengurumwa ameyasema hayo leo Ijumaa Mei 13, 2022 wakati akifungua mkutano wa maadhimisho ya miaka 10 ya mtandao huo ulioanzishwa rasmi mwaka 2012 na unatarajiwakuhudhuriwa na Rais Samia.
Amesema leo wanatarajia kuzindua taarifa yao ambayo itaweka wazi kwa miaka 10 wamefanya nini na wanatarajia kufanya nijnkwa miaka ijayo.
Hata hivyo alisema katika maadhimisho hayo pia kutakuwa na ripo nyingine inayozungumzia hali ya utetezi wa haki za binadamu Tanzania mwaka 2021 ambapo amesema itaeleza hali ilivyokuwa huko nyuma na kubainisha matukio yaliyotokea na uvunjifu wa haki za binadamu.
Naye Wakili wa THRDC, Leopod Mosha amesema hali ya Watetezi wa haki za binadamu nchini imeendelea kuimarika mwaka hadi mwaka licha ya uwepo wa changamoto mbalimbali.
Hata hivyo amesema katika kipindi cha miaka 10 jumla ya watu 400 wamepatiwa msaada wa kisheria ambao uliwasaidia watetezi kuweza kupata haki zao ndani ya mahakama.
“Mtandao pia umekuwa ukiwajengea uwezo watetezi wa haki za binadamu katika eneo la kisheria, lakini katika kipindi cha miaka 10 jumla ya waandishi wa habari 509 wamepatia mafunzo na kusaidiwa pale wanapopata changamoto mbalimbali katika kazi zao,” amesema
Kwa upande wake Balozi wa Marekani, Donald Wright ameuomba mtandao wa THRDC kuendelea kufanya kazi ya utetezi wa haki za binadamu na kusimamia upatikanaji wa haki miongoni mwa jamii.
Naye Katibu Mkuu wa Chama cha ACT-WAZALENDO, Ado Shahibu amesema wakati wakiadhimisha miaka 10 ni muhimu kupatikana kwa Katiba mpya ili kujenga misingi ya ufanyaji kazi za watetezi wa haki za binadamu.




