ACT WAZALENDO YAICHAMBUA BAJETI YA SERIKALI 2022/23
Bwana Emmanuel Mvula ambaye ni Msemaji wa Sekta ya Fedha na Uchumi wa ACT Wazalendo akifafanua jambo wakati akiwasilisha uchambuzi wa hotuba ya Bajeti Kuu ya Serikali kwa mwaka 2022/2023 jijini Dar es Salaam.
Kiongozi Mkuu wa Chama cha ACT Wazalendo Zito Kabwe akizungumza katika uwasilishaji wa uchambuzi kuhusu hotuba ya Bajeti Kuu ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2022/2023.
UCHAMBUZI WA BAJETI YA SERIKALI 2022/23 – ACT WAZALENDO
1.0 Utangulizi:
Siku kadhaa zilizopita, Serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan imewasilisha Bungeni Bajeti yake ya mwaka 2022/2023. Matarajio ya watanzania wote ni kuwa na bajeti inayoakisi maisha yao ya kila siku – ambayo kwa mwaka uliopita, wananchi wamelia na kodi lukuki, tozo, ongezeko la gharama za Maisha.
Aidha, wasilisho la bajeti ya awamu ya sita imetupa watanzania wote fursa ya kutathmini maono, malengo na ahadi za Serikali ya CCM.
ACT Wazalendo kama chama mbadala, tumekuwa na utamaduni wa kuzichambua bajeti za Serikali, kutathmini hali ya uchumi wa nchi na kuongea na wananchi tukilinganisha kama kuna uhalisia.
Tunafanya hivyo kwa kupima ahadi zinazotolewa kwa wananchi, shabaha za Serikali kwenye utekelezaji wake na kama kuna uwiano wa rasilimali fedha unaoelekezwa kwenye maeneo husika.
Ni vyema kurejea kuwa, hii ni bajeti ya pili chini ya Serikali ya awamu ya sita ambapo iliiidhinishiwa jumla ya shilingi 37.99 trilioni (mwaka 2021/2022) na mwaka 2022/2023 Serikali inaliomba Bunge kuidhinishiwa jumla ya Shilingi Trilioni 41.5.
Uchambuzi wetu ACT Wazalendo, umepima jinsi Serikali ya awamu ya Sita inavyojipambanua ikizingatiwa kwamba, Serikali hii ni matokeo ya Serikali ya awamu ya tano ambapo kama nchi tulipitia gizani kwa kushuhudia uongozi uliothamini vitu na kuliko watu wake, matumizi ya fedha yaliyokiuka taratibu na sheria za nchi na kupaa kwa deni la taifa.
Uchambuzi wetu umebaini kwamba, bajeti ya awamu ya sita Serikali
Bado Hakijaeleweka ni kipi inalenga hasa. Mwaka wa bajeti uliopita 2021/2022 mikakati yake ya kukusanya mapato imekuwa ikiyumba, matumizi yake hayatoi maendeleo ya wananchi kipaumble, imeendelea kukopa na kuongeza deni la taifa, kuwatwika wananchi mizigo ya tozo mpya kila kukicha na Serikali kushindwa kuwajibisha wanaoisababishia hasara.
Katika uchambuzi huu, ACT Wazalendo tumeangaza kwenye maeneo tisa (9) ambayo yanaonyesha ni dhahiri bajeti ya Serikali ya awamu ya Sita bado haijaeleweka na jinsi wananchi wanavyoendelea kupotoshwa na Serikali ya CCM:
1. MALENGO YA MAKUSANYO YA BAJETI YA 2021/22 HAYATOFIKIWA:
Katika mwaka wa fedha wa 2021/2022, Serikali iliidhinishiwa na Bunge kutumia jumla ya shilingi 37.99 trilioni. Taarifa ya Hali ya Uchumi ya 2021 iliyosomwa bungeni na Waziri wa Fedha Juni 14, 2022 inaonyesha kuwa mpaka mwezi Aprili 2022 shilingi 29.84 trilioni, sawa na 78.5% ya malengo, na iko chini ya malengo kwa 21.5%. Ni dhahiri kuwa bado hata kwa miezi miwili iliyobakia bado Serikali itakusanya chini ya malengo kwa tarakimu mbili.
Sababu zilizosababisha kutokufikiwa kwa malengo ya makusanyo ya mwaka wa fedha wa 2021/22:
i. Kupungua kwa mapato yasiyo ya kikodi kulikotokana na kupungua kwa usafirishaji wa Fedha kwa njia za kieletroniki (mobile money transfer) kwa sababu ya Tozo za miamala zilizowekwa.
ii. Kutokupatikana kwa kiasi kilichopangwa cha mikopo yenye masharti ya kibiashara.
Sababu ya kwanza inaonyesha athari za tozo za miamala ya simu zilizowekwa, huko mbeleni tutalieleza kwa kina hili.
Sababu ya 2 inaonyesha athari za kukopa sana mikopo ya kibiashara kwa miaka mitano iliyopita, jambo ambalo limepelekea mabenki ya kibiashara kuogopa kuikopesha zaidi Tanzania, tutaelezea hili zaidi.
2. FEDHA ZA BAJETI YA 2022/23 ZINAKWENDA WAPI?
Kwa mwaka wa fedha 2022/2023 Serikali imepanga kutumia jumla ya fedha Shilingi Trilioni 41.5. Mgawanyo wa matumizi wa fedha za serikali kwa mwaka wa fedha 2022/23 unaonyesha kuwa shilingi Trilioni 26.47 imetengwa kwa ajili ya matumizi ya kawaida ambayo sawa na asilimia 63.8. Wakati miradi ya maendeleo imetengewa Shilingi Trilioni 15.01 sawa na 36.2%.
Sehemu kubwa ya Bajeti ya mwaka 2022/23 inaenda kugharamia maeneo yafuatayo;
• Mishahara na Matumizi mengine ni shilingi trilioni 14.93 sawa na 39%.
• Gharama za kuhudumia Deni la Serikali ni shilingi Trilioni 9.1 sawa na 22% ya fedha zote.
• Michango ya Hifadhi ya Jamii na malipo mengne ni 5%
• Bajeti ya miradi ya maendeleo ni shilingi Trilioni 15.0 sawa na asilimia 36.2
Mgawanyo wa bajeti ya Maendeleo uliopelekwa kwenye matumizi ya Maendeleo ya wananchi ni kiwango kidogo zaidi. Ukiangalia bajeti ya maendeleo, kiwango kinachoelenga kuhudumia wananchi ni shilingi trilioni 6.2 sawa na 14.9% ya Bajeti yote ya 2022/23 ambazo mchanguo wake ni kama ifuatavyo: -
✓ Wizara ya Afya Shilingi Bilioni 555.13 (1.34%),
✓ Wizara ya Elimu Shilingi Bilioni 959.3 (2.31%),
✓ Wizara ya Tamisemi Shilingi Trilioni 3.26 (7.86%),
✓ Wizara Kilimo Mifugo na Uvivu Shilingi Bilioni 741.4 (1.79%),
✓ Wizara ya Maji Shilingi Bilioni 657.9 (1.59%)
✓ Wizara ya Maendeleo ya Jamii Shilingi Bilioni 11.09 (0.03%).
Sehemu kubwa ya Bajeti ya Maendeleo inayokwenda kugharamia vitu ni Shilingi Trilioni 6.6 sawa na 15.9 ya Bajeti yote ya 2022/23 ambazo mchanganuo wake ni kama ifuatavyo:-
• Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi Shilingi Trilioni 3.73 (8.99%),
• Wizara ya Nishati Shilingi Trilioni 2.68 (6.56%) na
• Wizara ya Ulinzi Shilingi Bilioni 230.33 (0.56%)
Mchanganuo huu wa matumizi ya mapato ya Bajeti ya mwaka 2022/23 unaonyesha kuwa sehemu kubwa ya Bajeti hii itatumika kulipa mishahara, kugharamia deni la Serikali, pamoja na matumizi mengine, huku 14.9% tu ya fedha zote za Bajeti ndiyo inayokwenda kwenye huduma za wananchi.
3. TOZO ZA MIAMALA YA SIMU NI MZIGO USIOBEBEKA KWA WANANCHI:
Mwenendo wa Makusanyo ya tozo za miamala ya simu kuanzia mwezi Julai 2021 hadi Machi 2022, unaonyesha kuwa Serikali imekusanya kiasi cha jumla ya bilioni 261 kati ya shilingi Trilioni 1.02 zilizotarajia kukusanywa. Makusanyo hayo ni sawa na asilimia 25.6 ya lengo la makusanyo yote ya miamala ya simu.
ACT Wazalendo tulitahadharisha kuwa kuanzishwa kwa tozo hizo kutaongeza maumivu makubwa sana kwa wananchi. Matokeo ya makusanyo haya kwa muda huo unaonyesha dhahiri kuwa tozo hizi ni mzigo usiobebeka kwa walipa kodi. Hivyo, kupelekea wananchi kupunguza kutumia huduma za miamala ya simu.
Aidha, hadi sasa bado kuna mkanganyiko kuhusu matumizi mahususi ya fedha zilizokusanywa kutoakana na tozo hizi.
Katika Hotuba ya Bajeti ya Serikali 2022/23 serikali imesema itapunguza makato/ada za miamala ya simu kwa asilimia 43. Punguzo hili haliwezi kuleta unafuu kwa wananchi.
Mapendekezo ya ACT:
1. ACT Wazalendo, tunaitaka Serikali ifute kabisa tozo za miamala ya simu irudi kama ilivyokuwa kabla ya mwezi Julai mwaka 2021 ili kuwapunguzia mzigo wananchi
2. Tunamshauri Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kufanya ukaguzi maalum wa matumizi ya fedha zote zilizopatikana kutokana na tozo za miamala ya simu. Ukaguzi huu ni muhimu sana kwani kuna mkanganyiko kuhusu matumizi ya fedha zilizopaswa kukusanywa kupitia miamala ya simu na fedha za mkopo wa Serikali wa kuimarisha uchumi kutokana athari za Ugonjwa wa Uviko-19 kutoka Shirika la Fedha Duniani (IMF).
4. DENI LA TAIFA: MIKOPO YA KIBIASHARA INALIGHARIMU TAIFA:
Kwa mujibu wa Hotuba ya Waziri wa Fedha na Mipango Bungeni, hadi
Aprili 2022, deni la Serikali lilikuwa shilingi trilioni 69.44, sawa na ongezeko la 14.4% ikilinganishwa na shilingi trilioni 60.72 Aprili 2021. Kati ya kiasi hicho, deni la ndani ni shilingi trilioni 22.37, sawa na 32.2% na deni la nje ni shilingi trilioni 47.07, sawa na 67.8%.
Katika deni la nje, deni lenye masharti ya kibiashara ni shilingi trilioni 14.27, sawa na 30.3%, deni hili pia lina malipo ya riba ya 2.5% kila mwezi, hivyo deni la kibiashara hubeba 32.8% ya deni lote la taifa, na huongeza kwa kiasi kikubwa matumizi ya nchi kwa kuwa tunalipa mikopo hata ya miradi ambayo haijaanza kufanya kazi (mfano mkopo wa Dola 1.5 Bilioni wa Benki ya Standard Chartered kwenye mradi wa Standanrd Gauge Railway).
Ukiondoa fedha za mkopo wa kibiashara tunaolipa, pia kwa mwaka Serikali inalipa Dola Milioni 700 kama riba ya mikopo yenye masharti ya kibiashara. Fedha hizi ni sawa na makusanyo ya mwezi mmoja ya TRA. Kwa ujumla Serikali hutumia shilingi trilioni 9.125 kugharamia malipo ya deni la Serikali. Hii ni sawa 22% ya bajeti yote ya nchi kwa mwaka 2022/23.
:
1. Serikali ipunguze uwiano wa mikopo ya kibiashara kwa deni la taifa mpaka kufikia asilimia 20 ya deni lote. Kwa sasa, Serikali ichukue hatua za kuangalia utaratibu wa kubadilisha madeni yenye masharti ya kibiashara kuwa madeni yenye masharti nafuu (concessional loans).
Kwa mfano Tanzania, kutokana na akiba yake (SDR), ina haki ya kupata mkopo nafuu kutoka Shirika la Fedha Duniani (IMF), kwa kiasi cha dola za kimarekani Bilioni 1.2 ambayo ni sawa na Shilingi Trilioni 2.7. Mkopo wa aina hii una riba sifuri, una muda wa mpito bila kulipa wa miaka kumi na hulipwa kwa muda mrefu mpaka miaka 30. Mkopo kama huu unaweza kupunguza madeni ya mikopo ya kibiashara ambayo tunayo kwa sasa na hivyo kuipa Serikali unafuu wa kulipa madeni ya kibiashara.
2. Serikali ipunguze uwiano wa mikopo ya kibiashara kwenye deni la Serikali hadi kufikia asilimia 20 ifikapo mwaka 2025. Hatua hii itapunguza mzigo wa Serikali kugharamia madeni, na hivyo kuipa unafuu Serikali kugharamia sekta zingine za Maendeleo ya wananchi kama vile afya, elimu, maji, umeme na kilimo.
5. KOROSHO: FEDHA ZA EXPORT LEVY ZIRUDI KWA WAKULIMA
1. Mwaka 2018 Serikali ilipora mapato yanayo tokana na ushuru wa mauzo ya nje ya korosho ghafi (Export Levy). Serikali ilibadilisha sheria na hivyo, kuchukua asilimia 100 ya mapato ya ushuru huu kwa ahadi kuwa Serikali ndio itakayohudumia gharama zote na haikufanya hivyo. Kabla ya mabadiliko haya asilimia 65 ya mapato yatokanayo na ushuru wa export levy yalikuwa yanarudi kwa wakulima kupitia mfuko wa kuendeleza zao la korosho.
Maamuzi ya kupora export levy yaliporomosha uzalishaji wa zao la korosho kiasi kwamba, Tanzania haijawahi kufikia tena kiwango kilichofikiwa mwaka 2018 cha tani 313,000.
Katika hotuba ya Bajeti mwaka 2022/23, Waziri wa Fedha amependekeza kuwa asilimia 50 ya mapato ya export Levy yaelekezwe Mfuko Mkuu wa serikali na asilimia 50 zingine kugharamia pembejeo kwa wakulima. Pendekezo hili la Serikali, licha ya nia njema inayoonekana kwa juujuu tu, ni mwendelezo wa kumkandamiza mkulima wa korosho.
Ni muhimu kukumbusha kuwa, dhana ya kuanzisha ushuru huu wa Export Levy kwenye Korosho isiyobanguliwa ni kuendeleza zao la korosho na sio chanzo cha mapato. Shabaha ya ushuru huu ni kuwezesha nchi kutouza tena nje ya nchi korosho ghafi kwa kuanzisha viwanda vya ubanguaji ndani ya nchi. Pendekezo la Waziri wa fedha halilengi kumsaidia mkulima bali linageuza ushuru huu kuwa chanzo cha mapato, hivyo ACT Wazalendo tunapinga kwa nguvu zote pendekezo hili.
Mapendekezo ya ACT Wazalendo:
1. Tunapendekeza Mfuko wa kuendeleza zao la Korosho urejeshwe na kupata mgawo wa 65% ya fedha za Export Levy ya Korosho kama ilivyokuwa kabla ya mabadiliko ya mwaka 2018.
2. Tunapendekeza Mfuko wa Maendeleo ya zao Korosho ufanyiwe marekebisho makubwa na kumilikiwa na wakulima wenyewe kupitia vyama vyao vya ushirika.
3. Tunapendekeza Fedha zinazokwenda kwenye mfuko wa kuendeleza zao la korosho zielekezwe kisheria kutumika kwenye maeneo yafutayo:
a. Kuanzisha skimu ya Hifadhi ya Jamii kwa wakulima wa Korosho, ambao mafao yake yatakuwa ni pamoja na bima ya afya kwa wakulima na Fao la Bei (price stabilization benefit), litakalohakikisha wakulima hawaathiriki pale ambapo bei ya zao hilo itakaposhuka kwenye soko la Dunia.
b. Kuendeleza Miundombinu ya maeneo yanayolima korosho. Ili kurahisisha usafiri na usafirishaji wa mazao na wananchi. Kwa mfano, Ujenzi wa barabara ya Korosho
(cashew ring road) [Nangurukuru – Liwale – Nachingwea –
Masasi – Newala – Tandahimba – Mtwara – Lindi – Nangurukuru] kutokana na mapato ya ushuru wa korosho kwa kutumia mfumo wa “development finance”.
c. Kuwezesha uanzishwaji wa viwanda vya ubanguaji korosho ili kuongeza mnyororo wa thamani wa zao la Korosho.
6. MGAWO WA FEDHA ZA MUUNGANO
Katiba ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Sura ya Saba Inazungumzia “MASHARTI KUHUSU FEDHA ZA JAMUHURI YA MUUNGANO”. Katika Sehemu ya Kwanza ya sura hii ya katiba Inaonyesha “MCHANGO NA MGAWANYO WA MAPATO YA JAMUHURI YA MUUNGANO”.
Ibara ya 133 ya Katiba hiyo, inaanzisha “Akaunti ya Fedha ya Pamoja”. Sharti hili liliingizwa kwenye katiba mwaka 1984, Lakini hadi leo akaunti hii haijaanzishwa. Aidha, Ibara ya 134(1) ya Katiba hiyo imeanzisha Tume ya Pamoja ya Fedha. Sheria namba 14 ya mwaka 1996 ilitungwa na Bunge ili kutekeleza kifungu hicho cha Katiba. Tume ilianzishwa mwaka 2003.
Kwa miaka zaida ya 36 tangu kutungwa kwa sheria ya kuanzishwa akaunti ya pamoja ya fedha za Muungano, akaunti hii bado haijaanza kufanya kazi na fedha zinazotokana na makusanyo ya Jamhuri ya Muungano yameendelea kutumika bila kujali haki na usawa wa pande mbili za Muungano.
Kwa mujibu wa utafiti uliofanywa na Serikali kupitia Kampuni ya ukaguzi wa mahesabu wa PwC, unaonyesha kuwa Zanzibar hutumia 2% tu ya Mapato ya Muungano (Yaani ni mapato ya Muungano yanayokusanywa Zanzibar) na Tanzania Bara hutumia 98% ya Mapato ya Muungano (yanayokusanywa Tanzania Bara). Utafiti huo ulitumia Bajeti za Serikali za kuanzia mwaka 1999 – 2004.
Utafiti huu pia umeonyesha kwamba, Katika mapato yanayokusanywa kutoka kwenye mambo ya Muungano, Matumizi yake ni asilimia 32 na asilimia 68 zinazobakia ni ziada. Fedha hizi zinapaswa kugawanywa kwa pande mbili za Muungano kwa kanuni maalum.
Kanuni ya mgawo wa fedha hizo ni asilimia 4.5 kwa Zanzibar na asilimia 95.5 kwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Kanuni hii ya mgawo wa 4.5% unatokana na ushauri wa IMF na kupitishwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania chini ya Waziri Mkuu John Samwel Malecela mwaka 1994. Kanuni hii ndio inayotumika hivi sasa kugawana Mikopo na Misaada kutoka nje baina ya pande mbili za Muungano.
Kwa kutumia mgawo wa 4.5%, Wastani wa Fedha zinazopaswa kuwa mgawo halali wa Zanzibar kwa miaka 8 iliyopita ni shilingi Bilioni 660 kwa mwaka tangu 2013/14 – 2021/2022. Huu ni mgawo wa ziada ya mapato yanayotokana na mambo ya Muungano baada ya matumizi ya shughuli za Muungano. Hata hivyo, Zanzibar hajawahi kupata mgawo wake halali kwa sababu hakuna akaunti ya pamoja ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kama ilivyoelekezwa na Katiba.
Hali hii inapelekea migogoro, manung’uniko na malalamiko makubwa ya mara kwa mara ya watu wa Zanzibar kuhusu haki zake ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Mapendekezo ya ACT Wazalendo:
1. ACT Wazalendo Inaitaka Serikali Kufuata Katiba ya Nchi kwa Kuanzisha Akaunti ya Pamoja ya Fedha kwa Mujibu wa Sheria na Mapato yote ya Muungano yawekwe humo.
2. Serikali ifanye utafiti mpya wa Mapato ya Muungano na Matumizi ya shughuli za Muungano ili kupata takwimu za sasa.
3. Serikali igawe ziada za mapato ya Muungano kwa Washirika wa
Muungano kwa mujibu wa Kanuni ya Mgao uliokubalika na Pande zote mbili.
4. Tunamshauri CAG Kufanya Ukaguzi maalum wa Fedha za Muungano, Mapato, Matumizi na Fedha zinazobakia, ili Kubainisha mgao sahihi na fedha ambazo Zanzibar inastahiki.
Kwenye Bajeti ya Serikali ya mwaka 2022/23 Serikali imebakiza kodi zile zile kwa wafanyakazi (PAYE) na Tozo za kuendeleza ujuzi (SDL) kama ilivyo kwenye Bajeti ya mwaka 2021/22. Waajiri wa sekta binafsi wataendelea kulipa SDL kwa kiwango cha asilimia 4 ya gharama za mshahara na wafanyakazi wa kima cha chini sasa watapaswa kulipa PAYE tofauti na utaratibu wa miaka yote ya nyuma.
Uamuzi huu wa kutorekebisha viwango vya kodi kwa wafanyakazi na waajiri inaondoa unafuu uliotarajiwa baada ya uamuzi wa Serikali kupandisha mishahara kwa wafanyakazi. Pia, kodi ya SDL inalipwa na waajiri wa sekta binafsi pekee wakati pia Serikali ni mnufaika wa wahitimu waliofadhiliwa na chanzo hiki cha mapato.
Mwaka 2016 Serikali ilifanya marekebisho ya sheria ya bodi ya mikopo na kuongeza makato ya kiwango cha marejesho kutoka 8% ya mshahara wa mdaiwa aliyeajiriwa kwa mwezi na hadi kufikia 15%. Makato hayo yamekuwa ni mzigo mkubwa kwa vijana wanaohitimu vyuo vya elimu ya juu.
Mapendekezo ya ACT Wazalendo:
1. Kodi ya kuongeza Ujuzi (Skills Development Levy – SDL) ishushwe mpaka 2%. Pia, wigo wa kodi hii upanuliwe kwa Serikali na Taasisi zake kulipa SDL kama ilivyo kwa waajiri wa sekta binafsi.
2. Tunapendekeza viwango vipya vya Kodi ya mapato (PAYE) ili kuendelea na utaratibu uliopo wa watu wenye kipato chini ya kima cha chini cha mshahara kutokulipa kodi hiyo.
Viwango hivyo vipya tunavyovipendekeza ni kama ifuatavyo:
MAPENDEKEZO YA ACT WAZALENDO YA VIWANGO VIPYA VYA KODI YA MAPATO
Mapato Kiwango cha Kodi Mapato ya Jumla yasiyozidi TZS 420,000 0%
Mapato ya Jumla yanayozidi 420,000 lakini hayazidi 720,000 TZS 36,000 + 8% ya Kiasi Kinachozidi TZS 420,000
Mapato ya Jumla yanayozidi 720,000 lakini hayazidi 1,440,000 TZS 72,000 + 15% ya Kiasi
Kinachozidi TZS 720,000
Mapato ya Jumla yanayozidi 1,440,000 lakini hayazidi 2,880,000 TZS 144,000 + 20% ya Kiasi Kinachozidi TZS 1,440,000
Mapato ya Jumla yanayozidi 2,880,000 lakini hayazidi 15,000,000 TZS 288,000 + 25% ya Kiasi Kinachozidi TZS 2,880,000
Mapato ya Jumla yanayozidi 15,000,000 TZS 3,000,000 + 30% ya
Kiasi Kinachozidi TZS
15,000,000
3. Serikali ianzishe kodi ya zuio (withholding tax) ya 10% kwa mapato yanayotokana na Posho za Vikao (Sitting Allowance).
4. Tunapendekeza Serikali ifanye Mabadiliko ya sheria ya Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu ili kurejea makato ya 8% ya kulipa mkopo wa elimu ya juu kama ilivyokuwa kabla ya mwaka 2016.
8. MASHIRIKA YA BIMA YA ZIC NA NIC YAENDELEE KULINDWA:
Katika hotuba ya Bajeti iliyosomwa na Waziri wa Fedha, ametoa tamko la kuifungua biashara ya Bima kuwa mali za Serikali na kuwa ya Ushindani. Utaratibu uliopo sasa unailazimu Serikali, Mashirika ya Umma na taasisi za Serikali kukata bima, kufanya hivyo kupitia Shirika la Taifa la Bima (NIC) na Shirika la Bima La Zanzibar (ZIC). Tamko la Waziri linaruhusu Serikali Kuu, Mashirika ya Umma, Asasi na Taasisi za Serikali sasa kukata Bima kwenye Mashirika binafsi ya Bima.
Biashara ya Bima ni adhimu sana kuachwa kwenye ushindani. Ifahamike kwamba, duniani kote kuna Mashirika ya Bima kama ilivyo kwa Hifadhi ya Jamii na ni chanzo kikubwa cha mtaji kwa serikali. Ni chanzo cha Serikali kupata mtaji wa kufanya uwekezaji, pia ni chanzo cha mapato cha wazi na kisicho na mawaa. Nchi nyingi duniani bado hazijaweka Bima kwenye ushindani wa soko huria. India kwa mfano; bado hawajaruhusu ushindani katika bima kwenye shirika la bima la Taifa kupata Biashara ya Serikali.
Mapendekezo ya ACT Wazalendo:
1. Tunapendekeza kuwa tamko la waziri wa fedha lifutwe kwa kuwa halina tija kwa Serikali na nchi.
2. Tunapendekeza magari yote ya Serikali yakatiwe Bima Kubwa (Comprehensive insurance). Kwa kuwa idadi ya magari ya Serikali itapungua kutokana na tamko la Waziri wa fedha kupunguza idadi ya magari ya Serikali, hakuna sababu tena ya magari hayo ya Serikali kutokukatiwa Bima kubwa.
3. Serikali na taasisi zake ziendelee kupata huduma ya bima kupitia mashirika ya NIC na ZIC tu.
9. TUNATAKA UWAJIBIKAJI ULIOSABABISHA HASARA KWENYE SAKATA LA KOROSHO 2018:
Mwaka 2018 Serikali iliingilia soko la zao la korosho kwa hatua za kununua zao hilo badala ya kuacha utaratibu wa kawaida wa minada kama ilivyozoeleka. Ili kutekeleza hatua hii, Benki ya Kilimo nchini (TADB) ilikopa shilingi bilioni 208 kwa ajili ya kununua korosho hizo. Fedha za mauzo hazikurudi kwa kuwa korosho husika ilikosa soko, na hivyo fedha hizo kupotea.
Katika Taarifa ya Hali ya Uchumi wa Taifa kwa mwaka 2021 iliyosomwa Bungeni, Waziri wa Fedha ametangaza kuwa Serikali imelibeba deni hili la TADB ya fedha hizi shilingi bilioni 208 ambazo zilikopwa kutoka benki ya Maendeleo ya Afrika (AFDB), kwa kuligeuza kuwa mtaji wa TADB.
ACT Wazalendo, kwanza tunataka uwazi na uwajibikaji kufuatia uamuazi uliopelekea hasara hiyo kubwa katika zao la korosho.
Hitimisho:
Tunamalizia kwa kuungana na kuwapa pole wananchi ambao bajeti hii inaendelea kuwaweka njia panda huku Serikali ikikwepa kugawana nao mzigo wa ongezeko la gharama za maisha. Tunaitaka Serikali kuacha kuwaadaha wananchi na sababu nyepesi za vita ya Urusi na Ukraine, janga la UVIKO-19 na badala yake kuweka mikakati madhubuti kuwaondoa wananchi kwenye ugumu wa gharama za maisha na hatimaye waondokane kuishi kwa taabu na umasikini.
Nchi yetu inazo rasilimali nyingi na uwezo wa kutoka kwenye mikwamo ya kiuchumi endapo Wananchi wataamka na kukataa muendelezo wa uwongo wa Serikali ya CCM ambayo kila bajeti yake haiakisi hali halisi ya maisha ya mtanzania mkulima, mvuvi, mwendesha pikipiki, bajaji, mama ntiliye, mfanyabiashara; vijana kwa wazee.
Nichukue fursa hii kuvishukuru vyombo vya Habari kwa kufuatilia chambuzi zetu kama chama mbala katika kipindi chote cha bajeti ambapo Wasemaji wa Kisekta wa ACT Wazalendo tuliwasilisha chambuzi za bajeti za kila wizara.
Uchambuzi wetu wa bajeti unahitimisha kwamba, Bado Hakijaeleweka!
Asanteni kwa kunisikiliza.
Imeandaliwa na:
Ndugu Immanuel Mvura emvula@actwazalendo.or.tz
Waziri Kivuli wa Fedha na Uchumi – ACT Wazalendo
16.06.2022


~2.jpg)


