TAMASHA LA BAGAMOYO 2022 KUWA KUBWA ZAIDI
Serikali imesema Tamasha la Kimataifa la Utamaduni na Sanaa Bagamoyo mwaka huu litakuwa kubwa zaidi na litaakisi neno “kimataifa.”
Akizungumza na Kamati ya Kuratibu Tamasha hilo iliyoteuliwa hivi karibuni na Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe Mohammed Mchengerwa, Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Dkt. Hassan Abbasi, aliyekutana na Kamati hiyo leo mjini Bagamoyo amesema Kamati hiyo imeaminiwa na ifanye mageuzi makubwa na ya haraka.
“Mwaka jana tuliweka viwango vya Tamasha hili lakini mwaka huu tunataka kuzidi viwango vile; ubunifu hauna ukomo wala hauna mwisho,” alisema Dkt. Abbasi.
Naye Mkuu wa Wilaya mwenyeji wa Tamasha hilo la Bagamoyo, Zainab Abdallah, amesema wanaBagamoyo wako tayari kushirikiana na Kamati hiyo kwani wao kiuchumi na kijamii ndio wanufaika wakubwa na wa kwanza wa Tamasha hilo.






