Breaking News

MISS WORLD TANZANIA 2026 WAAPA KUIBRAND SGR NCHINI VIETNAM

Walimbwende 20 wanaoshiriki kinyang’anyiro cha kumsaka mrembo wa Tanzania (Miss Tanzania) watakayepata nafasi ya kuiwakilisha nchi katika mashindano ya ulimbwende duniani, yanayotarajiwa kufanyika nchini Vietnam kati ya Agosti na Septemba 2026, wameahidi kuitangaza Reli ya Kisasa ya SGR kimataifa.

Ahadi hiyo waliitoa Machi 13, 2026 waliposafiri kwa kutumia treni ya SGR kutoka Dar es Salaam kwenda Dodoma, safari iliyolenga kuwapa uzoefu na kupanua upeo wao kuhusu maendeleo ya miundombinu nchini.

Mkurugenzi wa Taifa wa shindano hilo, Mustafa Hassanali, akizungumza mara baada ya kuwasili Dodoma, alisema kuwa uamuzi wa kutumia usafiri wa SGR umetokana na dhamira ya kuitangaza Tanzania kupitia jukwaa la Miss World. Alieleza kuwa lengo ni kuonesha kuwa Tanzania si nchi yenye vivutio vya asili pekee, bali pia ina miundombinu ya kisasa na salama.

“Miss World ni jukwaa la kimataifa la kuitangaza nchi. Mashindano haya hushirikisha zaidi ya nchi 100 na hufuatiliwa na mamilioni ya watu duniani. Kupitia fursa hii, nchi huonesha utamaduni, vivutio vya utalii, maendeleo ya kiuchumi pamoja na miundombinu,” alisema Hassanali.

Kwa upande wao, baadhi ya walimbwende walioshiriki safari hiyo walieleza kufurahishwa na huduma za SGR na kuahidi kuinadi kimataifa, hususan nchini Vietnam ambapo mashindano hayo yatafanyika.

Silya Mussa, mmoja wa washiriki wa Miss Tanzania, aliipongeza serikali kwa ujenzi wa reli ya SGR akisema imechochea ukuaji wa sekta mbalimbali ikiwemo utalii. Aliahidi kuwa, kama kijana, ataitangaza reli hiyo katika mashindano ya kimataifa.

Naye Christina Mbaga alisema kuwa endapo atafanikiwa kutwaa taji la Miss Tanzania, ataipa kipaumbele kuitangaza SGR sambamba na vivutio vingine vya utalii kama mbuga za wanyama, mito na rasilimali madini.

Kwa ujumla, huduma za SGR zimeendelea kuwa chachu muhimu katika kukuza sekta mbalimbali nchini, hivyo ni jukumu la kila Mtanzania kushiriki katika kuitangaza miundombinu hii kimataifa.