TMA YATOA ELIMU YA HALI YA HEWA KWA WAANDISHI WA MKOA WA DAR (DCPC)
Mchambuzi wa Hali ya Hewa kutoka mamlaka ya Hali ya HEWA TMA, Bi. Joyce Maketa Akifafanua jambo katika warsha hiyo ya waandishi wa habari mkoa WA Dar es salaam (DCPC).
Meneja Mahusiano wa TMA, Bi. Monica Mutoni akielezea katika warsha hiyo namna mamlaka hiyo inavyotekeleza majukumu yake hususani ushirikiano wa mamlaka hiyo na waandishi wa habari.
Dar es salaam:
Wanachama wa Chama Cha Waandishi wa Habari Mkoa wa Dar es Salaam (DCPC) Leo wamepatiwa mafunzo kuhusu shughuli zinazofanywa na Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA).
Mafunzo hayo yametolewa na Mchambuzi wa Hali ya Hewa Bi. Joyce Maketa katika mkutano wa DCPC na wadau mbalimbali ambapo amesema TMA inatoa taarifa za hali za maeneo mbalimbali ikiwemo sekta ya maji, kilimo na ujenzi.
Aidha amesema utoaji wa taarifa hizo unasaidia kujua ni wakati gani sahihi wa wakulima kulima na mazao ya aina gani yanafaa kupanda Kwa kipindi husika.
Ameongeza kuwa TMA pia inafanya tafiti zinazohusu Hali ya Hewa ambapo kwa sasa Kuna jambo kubwa linaloendelea duniani hivyo sio Tanzania tu inayoathirika na Mabadiliko ya Tabianchi lakini pia Mabadiliko ya Hali ya Hewa hivyo wao kama Taasisi ya serikali wanawajibu wa kufanya tafiti za Hali ya Hewa.
Akizungumza suala la El-nion ambayo ni ongezeko la joto katika eneo la Pasifiki amesema mfumo huo unasababishwa baadhi ya maeneo kuwa mvua kubwa ikiwemo Tanzania na mengine kuwa na upungufu wa mvua ikiwemo Afrika Kusini.
Awali akizungumza kuhusu ushiriki katika mkutano huo Meneja Mahusiano wa TMA Monica Mutoni amesema ushirikiano kati ya waandishi wa habari na Mamlaka hiyo ni WA muhimu kwani unawezesha wananchi kupata taarifa mbalimbali kuhusu Hali ya Hewa.
Hata hivyo amesema wataendelea kushirikiana na waandishi wa habari katika kuhakikisha kuwa wananchi wanapata taarifa sahihi na za uhakika zinazotolewa na Mamlaka hiyo.






