VIJANA WA VYAMA PINZANI WAPINGA WAKURUGENZI, MAAFISA NA WATENDAJI KUSIMAMIA UCHAGUZI, WAJA NA MAPENDEKEZO 16
Katibu wa Vijana CUF taifa Iddi Mkanza akisoma tamko la pamoja la Jumuia za vijana wa vyama pinzani Tanzania kupinga miswada ya sheria ya uchaguzi, tume huru ya uchaguzi na vyama vya siasa iliyosomwa kwa mara ya kwanza bungeni 10 Novemba 2023,katika mkutano na waandishi wa habari uliofanyika jijini Dar es salaam.
Mwenyekiti wa Ngome ya Vijana - ACT Wazalendo Taifa, Abdul Nondo akifafanua jambo katika tamko la pamoja la Jumuia za vijana wa vyama pinzani Tanzania kupinga miswada ya sheria ya uchaguzi, tume huru ya uchaguzi na vyama vya siasa iliyosomwa kwa mara ya kwanza bungeni 10 Novemba 2023, katika mkutano na waandishi wa habari uliofanyika jijini Dar es salaam.
Katibu wa vijana wa NCCR Mageuzi Taifa, Elisante Ngoma akitoa sababu za Jumuia za vijana wa vyama pinzani Tanzania kupinga miswada ya sheria ya uchaguzi, tume huru ya uchaguzi na vyama vya siasa iliyosomwa kwa mara ya kwanza bungeni 10 novemba 2023, katika mkutano na waandishi wa habari uliofanyika jijini Dar es salaam
Dar es salaam
Jumuia za Vijana wa vyama vya upinzani Tanzania wametoa tamko la kupinga miswada mitatu ya sheria iliyosomwa bungeni kwa mara ya kwanza novemba 10, 2023. Ambayo ni sheria ya sheria ya uchaguzi, tume ya uchaguzi na vyama vya siasa.
Akisoma tamko hilo kwa niaba ya Vijana hao kutoka katika Vyama vya ACT Wazalendo, CUF na NCCR Mageuzi katibu wa vijana CUF Taifa Iddi Mkanza amesema wanaipinga miswada hiyo mitatu kutokana na kuwa na kasoro na madhaifu makubwa mengi ikiwa ni pamoja na kutokubeba hoja zenye ustawi kwa vijana nchini.
"Sisi viongozi wa Jumuia za Vijana vyama vya pinzani nchini tunaamini wajibu wetu mkubwa ni kulinda na na kutetea maslahi ya vijana na ustawi wa vijana, kulinda ustawi wa demokrasia yetu pamoja na kuongeza hamasa na ushiriki wa vijana katika masuala ya kisiasa, kijamii na kiuchumi kwa lengo la kuwa na uwajibikaji madhubiti" alisema na kuongeza
"Sisi kama wawakilishi wa vijana tunao wajibu pia wa kupigania hali na usawa ili kudunisha amani ya nchi yetu. Kwani matatizo yoyote aidha kisiasa, kiuchumi au kijamii yatakoikumba nchi yetu waathirika wakubwa ni vijana kutokana na kuwa wao ni zaidi ya asilimia 70 ya idadi ya watu wote nchini"
Alisema wameichambua kwa kina miswada hii na kubaini kasoro na mapungufu na madhaifu makubwa vifungu vingi vya miswada hii vimekinzana na katiba ya JMT 1977, kwa Kutoleta usawa na haki nchini hivyo kutokuimarisha demokrasia na kupanua ushiriki wa kisiasa wa wananchi, vijana na makundi mengine.
Ameyataja maeneo kumi yenye mapungufu kuwa ni pamoja na;
kwanza ni wakurugenzi wa jiji, Manispaa, Miji na Halmashauri pamoja na watumishi wa umma kuendelea kuwa wasimamizi wa uchaguzi ambapo kifungu cha 6(1) cha muswada wa sheria ya uchaguzi kinatoa fursa kwa wakurugenzi wa majiji, manispaa, miji, Halmashauri na watumishi wa umma katika kifungu cha 6(2) kuwa wasimamizi wa uchaguzi ngazi ya jimbo na kata
Pili namna ya upatikananji wa mwenyekiti na makamu mwenyekiti wa tume, muundo wa Tume ya uchaguzi na sifa za wajumbe wa Tume ambapo kamati ya usaili yenye jukumu la kuchakata na kusimamia mchakato wa usaili, mamlaka yake yanaishia kwa wajumbe wa tume ya uchaguzi kama ilivyoaimishwa katika muswada wa sheria mpya ya Tume ya uchaguzi kifungu cha 9(1) (5)(6)(7)(8) kuwa watakaoomba nafasi hiyo kuwa wajumbe wa Tume ya uchaguzi .
Tatu ni dhamana ya fedha inayowekwa na mgombea kwa msimamizi wa uchaguzi ambapo kifungu cha 35(1) (2)na 51(1) cha muswada wa sheria ya uchaguzi katika uchaguzi kitaka mgombea wa udiwani, ubunge au Urais kuweka dhamana ya fedha baada ya uteuzi na fedha hizo kitaifishwa ikiwa mgombea atapata moja ya kumi ya kura halali au mgombea kujitoa mara baada ya uteuzi.
Nne ni kuwekwa kwa zuio kwa asiyeridhika na maamuzi ya Tume kutokwemda mahakamani ( Ouster Clauses/ Finality Clauses/ Exclusionary clauses) katika miswada hii bado kuna vifungu ambavyo vianipa tume ya uchaguzi hivyo kipokonya mamlaka na wajibu wa mahakama kwamba maamuzi ha Tume ndio ya mwisho.
Tano tunasikitika kuwa miswada hii haijajumuisha hoja za vijana na maswala ya vijana ya muda mrefu hili kuamua wingo wa ushiriki wa vijana kisiasa na ikizingatiwa asilimia 70 ya idadi ya watu nchini ni vijana.
Sita tunauoinga muswada wa sheria ya uchaguzi kutojumuisha uchaguzi wa serikali za mitaa, vijiji na vitongoji katika muswada huu wa sheria ya uchaguzi unakumuisha uchaguzi wa Rais, wabunge na madiwani tu ambapo sheria hii inakuja kufuta sheria ya uchaguzi wa madiwani sara 292 na sheria ya Taifa ya uchaguzi sura 343.
Saba tunapinga kifungu kinachozuia wafungwa kutumia haki yao ya kupiga kura ambapo kifungu cha 10(1) C cha kuswada wa sheria ya uchaguzi kinazuia mtu aliyetiwa hatiani kwa kifungo kinachozidi miezi 6 na kifungo cha maisha kutokupiga kura.
Nane tunapinga fedha za uendeshaji wa shughuli za tume ya uchaguzi kutoka katika bajeti ya serikali katika kifungu cha 22 cha muswada wa sheria ya Tume ya uchaguzi kinazungumzia fedha za uendeshaji wa shughuli za Tume zaitatoka katika bajeti ya serikali yaani ofisi ya waziri mkuuna Tume ya uchaguzi kupangiwa ipewe shilingi ngapi na lini, kifungu hiki hakifai kwani kinadhoofisha uhuru wa Tume katika kutekeleza majukumu yake.
Tisa Tunapinga Tume ya uchaguzi kulipisha wananchi fedha kwa kadi ya kupuga kura iliyoharibika, kufutika au kupotea ili apewe kadi mpya, hii inajitokesha katika miswada wa sheria ya uchaguzi kifungu 20(1)(2) na 21 (2) ambacho kinasema ikiwa mtu atapoteza kadi ya kupiga kura au kadi hiyo kufutika au kuharibika basi ikidhibitishwa na afisa mwandikishaji mtu huyo atapewa kadi mpya baada ya kulipia ada.
Kumi mamlaka makubwa aliyopewa msajili wa vyama vya siasa na mwanasheria mkuu wa serikali katika kuweka mapingamizi dhidi ya wagombea katika miswada wa sheria ya uchagzuzi kifungu cha 37(3) ngazi ya rais, kifungu cha 53(3) ngazi ya ubunge na kifungu cha 65(3) ngazi ya udiwani vifungu hivi vinatoa uzito mkubwa wa kupitiliza watendaji wa serikali ka msajili wa vyama na mwanashria mkuu wa serikali kuweka mapingamizi kwa wagombea wa ngazi yoyote hivyo kuibua hisia za njama kwa vyama vua upinzani ikiwa ni pamoja na matumizi mabaya ya mapingamizi
MAPENDEKEZO YA JUMLA YA JUMUIYA ZA VIJANA VYAMA PINZANI KUHUSU MISWADA KUTOKA KWENYE TAMKO LA PAMOJA.
1.Vifungu hivi 6(1) na 6(2) katika muswada wa sheria ya uchaguzi vinavyohusu kutumia wakurugenzi wa Halmashauri na watumishi wa umma vifutwe vyote na hivyo kutoa fursa kwa Tume ya uchaguzi kuajiri watendaji wake yenyewe ,wenye sifa zitakazoainishwa kuanzia ngazi ya Mkoa ,Wilaya hadi Halmashauri kwa ajira za kudumu na za muda. Watu waombe kwa sifa,wafanyiwe usaili wa wazi badala ya Tume kutumia wakurugenzi wa Halmashauri.
2.Mwenyekiti na makamu mwenyekiti wa Tume na wao wanapaswa kupita kwenye mchakato wa kuomba na kufanyiwa usaili na kamati ya usaili kama wajumbe wengine wa Tume.
3.Kifungu cha 18(2) kirekebishwe ,Muundo wa Tume ya uchaguzi ugawike sehemu mbili yaani Bodi na Menejimenti , ambapo Bodi iwe chini ya Mwenyekiti wa Tume ambapo Bodi hii ndio inapaswa kufanya mchakato wa kuajiri Mkurugenzi wa uchaguzi kwa sifa zitakazo ainishwa na kwa uwazi .Mkurugenzi wa uchaguzi ndio atakuwa mtendaji Mkuu wa Tume ya uchaguzi na ataongoza Menejimenti katika utendaji wa kila siku.
4.Kifungu cha 9(3) kifutwe kumuondoa Mkurugenzi wa uchaguzi kuwa katibu wa kamati ya usaili na badala yake katibu wa kamati ya usaili awe Katibu Mtendaji wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora.
5. Sifa ya kutokuwa mwanachama au kujihusisha na chama cha siasa inapaswa iongezwe kwenye kifungu cha 7(1) na (2) cha muswada wa sheria ya Tume ya uchaguzi ili iendane na ibara ya 74(14) ya katiba ya JMT 1977.
6. kifungu cha 18(2)(d) cha muswada wa sheria ya Tume ya uchaguzi kifutwe ili kuondoa sifa ya Mkurugenzi wa uchaguzi kuwa Afisa muandamizi katika utumishi wa umma. Mchakato wa kumpata mkurugenzi ufanywe na Tume ya uchaguzi kwa uwazi kuruhusu mtu yeyote kuomba kulingana na sifa zingine zitakazoainishwa.
7.Sifa za wajumbe wa Tume katika kifungu cha 7(2) cha muswada wa sheria mpya ya Tume ya uchaguzi uzingatie vijana. Kifungu kitamke angalau wajumbe wawili kati ya watano wawe vijana.
8.Kifungu cha 35(1)(2) na 51(1) katika muswada wa sheria ya uchaguzi vifutwe sababu vipo kinyume na katiba JMT 1977 ibara ya 21(1)(2) inayoruhusu uhuru wa mtu kushiriki katika masuala ya kiuongozi na maamuzi. Pia kifungu hiki kinazuia ushiriki wa vijana, hivyo hakuna haja ya mgombea kuweka dhamana kwa msimamizi wa uchaguzi ni jambo ambalo halina mantiki, ikiwa mgombea amepitishwa na chama chake inatosha kumuamini badala ya kuweka vikwazo vya dhamana ya fedhha.
9.Tunapendekeza mgombea apewe haki kwa mujibu wa katiba JMT 1977 ibara ya 13(6)(a) kama hajaridhika na maamuzi ya Tume ya uchaguzi kukata rufaa na kupinga maamuzi hayo mahakama kuu. Kitendo cha kuzuia kukata rufaa ni kinyume pia na ibara ya 107(A) ya katiba ya JMT 1977 inayotoa mamlaka kwa mahakama kama chombo cha maamuzi ya mwisho katika utoaji haki ndani ya JMT. Pia kuzuia watu kukata rufaa kupitia mahakama ambayo ndiyo njia ya amani na usawa katika kutafuta haki tafsiri yake ni kuwatengenezea mazingira wananchi kutafuta haki yao kwa njia nyingine aidha barabarani au msituni jambo ambalo sio sahihi kwa ustawi na mustakabali wa nchi yetu.
10.Kuingizwe hoja za Vijana katika miswada hii, na tunapendekeza kama ifuatavyo.
➢ Muswada wa sheria ya vyama vya siasa haujazingatia hoja ya kulazimisha vyama vyetu vya siasa kuwa na asilimia kadhaa ya vijana katika hatua ya uteuzi wa wagombea wa ngazi ya udiwani na ubunge.Muswada utamke wazi kuwa 40% ya wagombea ndani ya vyama ngazi udiwani na ubunge wawe vijana.
➢ Muswada wa sheria ya vyama vya siasa unapaswa kulazimisha vyama vyetu kutenga asilimia kadhaa ya ruzuku inayotolewa kwenye chama itumike kuwezesha na kuhamasisha ushiriki wa vijana kwenye siasa kupitia shughuli na majukumu ya Jumuiya za vijana katika vyama.
➢ Muswada wa sheria ya uchaguzi na mabadiliko ya katiba ya 1977 inapaswa kuweka ukomo wa muda fulani katika kutumikia nafasi moja ya uongozi, ngazi ya udiwani na ubunge kama ilivyo nafasi ya urais.Muswada uweke ukomo wa miaka 10 wa mtu kutumikia au kugombea nafasi moja.
➢ Muswada wa vyama vya siasa na gharama ya uchaguzi unapaswa uweke kifungu cha kuilazimisha serikali kugharamia fedha za kampeni (Ruzuku)kwa wagombea wote vijana ili kupanua wigo wa ushiriki wa vijana.Katika uchaguzi wa 1995 iliwezekana wagombea kupewa ruzuku na Tume ya uchaguzi.
➢ Sifa za wajumbe wa Tume katika kifungu cha 7(2) cha muswada wa sheria mpya ya Tume ya uchaguzi izingatie vijana. Kifungu kitamke angalau wajumbe wawili kati ya watano wawe vijana. Pia asilimia kadhaa ya watendaji wa tume wawe vijana.
➢ Marekebisho ya muswada wa sheria ya uchaguzi na mabadiliko ya katiba ya 1977 ibara ya 67(1)(a) yafanyike kutoa fursa kwa kijana wa miaka 18 anayeruhusiwa kupiga kura pia awe na sifa ya kugombea nafasi ya udiwani hata ubunge na isiwe hadi umri wa miaka 21.
➢ Marekebisho ya muswada wa sheria ya uchaguzi na mabadiliko ya katiba ya 1977 ibara ya 39(1)(b) yafanyike ili kupunguza umri wa kugombea urais na makamu wa urais kutoka miaka 40 hadi 35 ili kutoa fursa kwa vijana wenye uwezo kutoa mchango wao wa maarifa katika kuongoza nchi kwa maendeleo na ustawi wa Taifa.
➢ Marekebisho ya muswada wa sheria ya uchaguzi na mabadiliko ya katiba ya 1977 ibara ya 66(1)(e) yafanyike ili uteuzi wa wabunge 10 wanaoteuliwa na Rais uzingatie vijana,sheria na katiba itamke wazi kwamba kati ya wabunge 10 angalau 4 wawe vijana jinsia ya kiume na kike.
➢ Muswada wa sheria ya vyama vya siasa upanue wigo kwa kuweka masharti kuvilazimisha vyama vyetu asilimia kadhaa ya wajumbe katika vikao vikubwa vya chama kama kamati kuu na Halmshauri kuu wawe vijana ili kupanua wigo wa ushiriki wa vijana.
➢ Marekebisho ya muswada wa sheria ya uchaguzi na mabadiliko ya katiba ya 1977 yafanyike kuruhusu mgombea binafsi na kuondoa sifa ya kuwa mwanachama tuu ili kugombea, hii itaongeza sana ushiriki wa vijana.
➢ Marekebisho yafanyike katika muswada wa sheria ya uchaguzi kifungu cha 85(1) na 14(1) kuruhusu wananchi kupiga kura ya Udiwani,Ubungen na Urais popote walipo hata kama ni tofauti na maeneo waliyojiandkishia ,hili linawezekana kupitia matumizi ya Tehama na Teknolojia katika chaguzi. Na itasaidia vijana wengi nchini hasa wanafunzi na diaspora wenye sifa ambao mara zote wanapoteza haki ya kupiga kura sababu wapo mbali na maeneo waliyoandikishwa kupiga kura.
11.Muswada wa sheria ya uchaguzi ujumuishe pia chaguzi za serikali ya mtaa(Neighborhood Elections) na uitwe Muswada wa sheria ya uchaguzi wa Rais,wabunge ,madiwani na viongozi wa serikali ya mitaa,vijiji na vitongoji.
12. Uchaguzi wa viongozi wa serikali ya mitaa,vijiji na vitongoji usimamiwe na Tume ya uchaguzi na sio Waziri wa TAMISEMI, hii ni kwa sababu Waziri wa TAMISEMI ni mwanachama wa CCM hana uhalali na utaalamu wa kusimamia uchaguzi na hawezi kuzingatia usawa kwa vyama vingine vinavyoshindana na chama chake cha CCM.
13.Kifungu cha 10(1)C cha muswada wa sheria ya uchaguzi kinachozuia wafungwa kupiga kura kinapaswa kifutwa sababu kina kinzana na ibara ya 5(1) ya katiba ya JMT 1977, pia kina kinzana na hukumu ya mahakamu kuu katika kesi No.3 ya 2022 ya Tito Magoti.
Lakini pia ulimwengu umebadilika sasa nchi nyingi duniani zinaruhusu wafungwa kupiga kura bila kikwazo. Miongoni mwa nchi hizo baadhi ni,Kenya,Denmark,Finland,France,Zibabwe,Japan,Poland,Peru,Norway,Netherlan ds,Ireland,Latvia,Lithunia,Spain,Sweden,Switzerland,CzechRepublic,Macedonia, Romania ,Cyprus na Ukraine.
14.Tunapendekeza fedha za kuendesha shughuli za Tume zitoke kwenye mfuko mkuu wa serikali (Consolidated Fund) ambazo ni fedha za uhakika,zenye utaratibu mzuri na ambazo haziguswi zikiingizwa huko ,hii itaongeza uhuru na ufanisi wa Tume katika kutekeleza majukumu yake tofauti na sasa hivi Tume ya uchaguzi inatengewa na kupewa fedha kama hisani kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu.
15. Tunapendekeza kuondoa gharama za kupata kadi /kitambulisho kipya cha mpiga kura.Tunapendekeza maneno “ada” yafutwe na kuondolewa ili kuongeza hamasa ya wananchi na vijana kupiga kura na pia ili kiende sambamba na matakwa ya katiba ya JMT 1977 ibara ya 5(1) na 21.
16.Tunapendekeza kuondoa mamlaka za serikali (Msajili wa vyama vya siasa na Mwanasheria Mkuu wa serikali) katika kuweka mapingamizi dhidi ya wagombea. kifungu kiruhusu mtu yeyote kuweka pingamizi na sio Ofisi ya Msajili wa vyama vya siasa au Mwanasheria Mkuu wa serikali.






