TANZANIA KUWA MWENYEJI SEMINA MAALUM KUHUSU MPANGO WA BIASHARA KATI YA UINGEREZA NA NCHI ZINAZOENDELEA
Dodoma,
Tanzania inataraji kuwa mwenyeji wa Semina maalum kuhusu Mpango wa Biashara wa nchi ya Uingereza na Nchi Zinazoendelea (UK Developing Countries Trading Scheme - DCTS) inatarajiwa kufanyika tarehe 28 Machi katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa jijini Dar es Salaam.
Kwa mujibu wa taarifa kwa vyombo vya habari imesema kuwa Semina hiyo ya siku moja itafunguliwa na Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (Mb) na kufungwa na Mhe. Omar Said Shabaan, Waziri wa Biashara na Maendeleo ya Viwanda, Zanzibar.
"Semina hiyo ina lengo la kufahamisha wadau wa biashara nchini juu ya fursa ya mauzo ya bidhaa za Tanzania katika soko la Uingereza kupitia Mpango wa Serikali ya Uingereza wa Kufanya Biashara na Nchi Zinazoendelea uliozinduliwa mwezi Mei mwaka 2023. Tanzania ni miongoni mwa nchi 65 ambazo Uingereza imezijumuisha katika mpango huo ili kuweza kuuza bidhaa zake bila kulipa ushuru na imeingia pia katika kundi la nchi ambazo asilimia 99 ya bidhaa zake zitanufaika na msamaha wa kodi".
Taarifa hiyo imeongeza kuwa walengwa wa semina hiyo ni wadau wa biashara wenye nia ya kuuza bidhaa za aina mbalimbali katika soko la Uingereza. Ambapo wadau ambao wapo nje ya mkoa wa Dar es salaam wataweza kushiriki katika Semina hiyo kwa njia ya mtandao, kupitia link maalum ya mtandao wa "Teams" itakayotolewa kwa watakaojisajili au kupitia https://docs.google.com/forms/d/e/1FAIpQLSdjoGDLwkXfu9PWIV7Oc3LOnn5tRyELsimZVUaMaFhCGFB1Mw/viewform
Aidha taarifa hiyo ilibaisha kuwa wananchi wote wanaweza kuifuatilia Semina hiyo kupitia na chaneli ya YouTube ya Ubalozi wa Tanzania nchini Uingereza ijulikanayo kamaUbaloziLondon(http://www.youtube.com/@ubaloziLondon).





