VIJANA WAASWA KUTUMIA MITANDAO YA KIJAMII KUINGIZA KIPATO
Vijana nchini wameaswa kutumia mitandao ya kijamii kujinufaisha kupitia maarifa yanayopatikana kwenye urithi wa asili na utamaduni kwa kuandaa maudhui mbalimbali yatakayowawezesha kujiingizia kipato kwa lengo la kujipatia maendeleo binafsi na ya Taifa kwa ujumla.
Wito huo umetolewa leo tarehe 23 Machi 2024 na Mkuu wa Idara ya Programu, Makumbusho na Nyumba ya Utamaduni, Bw. Chance Ezekiel katika Kongamano lililohusisha Makumbusho ya Taifa la Tanzania kupitia programu maalum ya 'Twenzetu Makumbusho Nyumba kwa Nyumba' kwa kushirikiana na asasi ya 'Vijana tunaongea' lililofanyika katika kituo cha Makumbusho na Nyumba ya Utamaduni jijini Dar es Salaam.
Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa Makumbusho ya Taifa, Bw.Chance amesema vijana wana nafasi kubwa na muda mwingi wa kutumia mitandao ya kijamii na kwamba ni vyema wakatumia mitandao hiyo kwa manufaa kuliko kupoteza muda mwingi kutazama vitu visivyo na tija na hatimaye kujiingiza kwenye tabia zinazoenda kinyume na maadili ya Mtanzania.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti baadhi ya vijana walioshiriki kongamano hilo wamesema wamejifunza namna ambavyo Makumbusho inafanya kazi ya kuhifadhi wa urithi wa asili na utamaduni kwa weledi na kuahidi kuendelea kushirikiana na Taasisi hiyo katika matukio mbalimbali yanayolenga kuendeleza utamaduni wa Mtanzania.
Vijana zaidi ya 500 kutoka vyuo vikuu mbalimbali vya jijini Dar es Salaam ikiwemo Chuo kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Chuo cha Usimamizi wa Fedha (IFM), Chuo Kikuu cha Kampala (KIU) na Chuo cha Bishara (CBE) na vinginevyo wamehudhuria Kongamano hilo ambalo litachagiza programu maalum ya 'Twenzetu Makumbusho Nyumba kwa nyumba' inayotarajiwa kuanza hivi karibuni.







