MATINYI: WANANCHI WANAOTAKA KWENDA MSOMERA WAFUATE UTARATIBU
Serikali Imewataka wananchi wanaoishi ndani ya Eneo la Hifadhi ya Ngorongoro, wanaotaka kwenda katika kijiji cha Msomera wafuate taratibu zote za kuhamia huko ili kuepuka usumbufu na changamoto mbalimbali hususani ya makazi na huduma zingine.
Rai hii imetolewa leo Mei 26, 2024 na Mkurugenzi wa Idara ya Habari (Maelezo) na Msemaji Mkuu wa Serikali, Mobhare Matinyi wakati akiongea na waandishi wa habari juu ya zoezi la kuhama kwa hiari wananchi wanaoishi katika eneo la hifadhi ya Ngorongoro amesema kuna taarifa kwamba baadhi ya watu kutoka Ngorongoro huenda Msomera kusalimia ndugu na jamaa zao na wakiona mazingira ni mazuri huamua kubaki huko.
"Kumekuwepo na taarifa kwamba baadhi ya watu kutoka Ngorongoro huenda Msomera kusalimia ndugu na jamaa zao na wakiona mazingira ni mazuri huamua kubaki huko na kusababisha changamoto ya makazi na huduma zingine". Alisema Bw. Matinyi.
Alisema Serikali inaendelea kuboresha makazi mapya na kuhamasisha uhamaji wa hiari ambapo amesisitiza na kushauri kuwa wale wote wanaotaka kuhamia kwa hiari kufuata taratibu zote zinazotakiwa hili kihamia huko.
Ametaja moja ya faida watakazozipata wakazi hao pindi watakapokamilisha taratibu zote za kuhama kwa hiari kuwa ni wakuu wa kaya huoneshwa fidia wanayostahili kulipwa mbali ya fedha za ziada ambazo Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan aliekeleza kila kaya ilipwe, yaani shilingi milioni 10.
Akizungumzia juu ya uthaminishaji na malipo stahiki alisema zoezi la Uhamaji hufanyika baada ya malipo ya fidia kukamilika, kuvunja makazi au maendelezo na kuchagua mali wanazotaka kuhama nazo. ndipo usafirishaji wa watu, mifugo na mali zao hufanyika kwa hiari na kuhakikisha wasafiri kupata huduma zote safarini hadi kufika Msomera au popote alipochagua kuhamia nchini mbali ya usafiri pia hulipwa shilingi milioni 15 za ziada kwa kila kaya badala ya shilingi milioni 10.
Bwana Matinyi aliongeza kuwa kwa wananchi wanaohamia sasa Msomera, na baadaye Kitwai na Saunyi, atapata hati za nyumba ya vyumba vitatu iliyo katika eneo lenye ukubwa wa ekari 2.5 na shamba binafsi la ekari tano. Hati hizi hukabidhiwa kwa wakuu wa kaya wakati wa kuagwa wakiwa Ngorongoro chini ya usimamizi wa Mkuu wa Wilaya, Mhe. Kanali Wilson Sakulo.
Alisema Wananchi hao watapewa chakula magunia mawili ya mahindi kwa kila kaya kwa muda wa miezi mitatu kwa muda wa miezi 18 wakati wakiandaa mashamba, malisho, majosho na maji ya mifugo yao. kujengewa shule za msingi na sekondari, vituo vya afya, mnada wa kisasa na vituo vya kuuzia maziwa, miundombinu ya maji, barabara, umeme, posta pamoja na mawasiliano.
Aidha bw. Matinyi alisema Serikali inawashauri wananchi wanaopatwa na changamoto zozote wawasiliane na serikali za vijiji au Mkuu wa Wilaya ya Handeni, Mhe. Albert Msando wahudumiwe wakati Serikali inaendelea kuboresha makazi mapya.




