Breaking News

RC CHALAMILA AZINDUA KAMATI YA UWEKEZAJI DSM

Dar es salaam 
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Mhe Albert Chalamila amezindua rasmi Kamati ya uwekezaji Katika Mkoa huo ambayo kwa kushirikiana na Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC ) itakuwa na jukumu la kuratibu na kusimamia mnyororo mzima wa uwekezaji na mwekezaji wa ndani au wa nje katika Mkoa huo.

Asema makuzi na uhamasishaji wa uwekezaji ni moja ya kipaumbele kikubwa cha Mhe Rais Dkt Samia Suluhu Hassan.

RC Chalamila alisema Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt Samia Suluhu Hassan ameweka nguvu kubwa katika makuzi na uhamasishaji wa uwekezaji hapa nchini hivyo kuundwa kwa kamati hiyo ni kuunga mkono Jitihada za Mhe Rais kwa masilahi mapana ya Mkoa wa Dar es Salaam na Tanzania kwa ujumla.
Aidha RC Chalamila alisema kamati hiyo waliweza kujadiliana maswala mbalimbali kwa lengo la kuweka mazingira rafiki kwa mwekezaji ikiwemo vikwazo vya kikodi na Sheria, mfumo mzima wa masoko, pamoja na ushirikishwaji wa wananchi na wadau mbalimbali wa uwekezaji.

Vilevile RC Chalamila aliitaka kamati hiyo kutekeleza malengo yake kwa ufanisi na kuzingatia masuala mbalimbali ya uzalishaji, usafirishaji, kuhakikisha uwekezaji endelevu wenye tija.
Sanjari na hilo Kamati hiyo ya uwekezaji ya Mkoa inaundwa na taasisi 15, Wajumbe 19, ambapo mwenyekiti wa Kamati hiyo ni Katibu Tawala wa Mkoa wa Dar es Salaam Dkt Toba Nguvila na Katibu wa Kamati ni Bwana Fidelis Obanga Kutoka TIC

Uzinduzi wa kamati hiyo umefanyika Juni 4,2024 makao makuu ya TIC Jijini dar es salaam.