CUF YAISHUKIA CCM KUHUSU UPOTOSHAJI JUU YA KUPOKEA WANACHAMA WAO DAR NA LINDI
CUF- Chama Cha Wananchi kinashangazwa na udanganyifu na vituko vinavyofanywa na viongozi waandamizi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) ambao waliwahi kuheshimika kwa sababu mbalimbali katika jamii.
Katika siku na maeneo tofauti Katibu wa Uenezi wa CCM ndugu Amos Makalla na Katibu Mkuu wa Chama hicho Dkt Emmanuel Nchimbi walijitokeza hadharani Dar es Salaam na Lindi na kuwapokea waliokuwa wanachama wa CHADEMA na ACT-Wazalendo na kwa makusudi wakatekeleza udanganyifu kwa Umma kwa kudai kwamba wamechukua wanachama wa CUF- Chama Cha Wananchi, ili kujitengenezea sifa za uongo.
Ndugu Abdul Kambaya aliyepokelewa na Makalla Makumbusho Dar es Salaam alikuwa mwanachama wa CHADEMA baada ya kufukuzwa kwa makosa ya kinidhamu kutoka CUF-Chama Cha Wananchi, kama ambavyo Ndugu Hamidu Bobali alijiunga mwanachama wa ACT- Wazalendo baada ya kuadhibiwa zaidi ya miaka miwili iliyopita.
Tunaamini kwamba Makalla, Nchimbi na viongozi wengine waandamizi ndani ya CCM wanafahamu kwamba wahusika hao hawakuwa wanachama wa CUF- Chama Cha Wananchi wakati wanawapokea kwa kuwa kujiunga kwao kwenye vyama hivyo kulikuwa bayana kutokana na ukweli kwamba Maamuzi ya CUF- Chama Cha Wananchi dhidi yao hayakufanyika gizani. Aidha, tunatambua kwamba kuwahusisha na CUF- Chama Cha Wananchi wahusika hao kulimaanisha kuwaongezea thamani na kuyapa uzito matukio hayo. Hata hivyo, ulaghai huo wa kitoto hatukuutarajia kuratibiwa na viongozi wa ngazi ya akina Makalla na Nchimbi.
Tunatoa wito kwa vyombo vya habari vyote vilivyoripoti UPOTOSHAJI huo kulirekebisha hilo kwa kuwahusisha wahamaji hao na vyama halisi vilivyowahusu. Aidha, tunatoa wito kwa wanachama na mashabiki wetu nchi nzima kujizatiti kwa ajili ya Maandalizi ya Uchaguzi wa Serikali za mitaa, vijiji na vitongoji unaotarajiwa kufanyika mwaka huu tangu ulipofanyika mara ya mwisho miaka 10 iliyopita.





