JAMII YASHAURIWA KUZINGATIA USHAURI WA WATAALAM WA AFYA KULINDA FIGO ZAO
Jamii imeshauriwa kuepuka unywaji wa pombe uliokithiri, matumizi ya tumbaku, matumizi holela ya dawa za kutuliza maumivu pamoja na dawa za kienyeji ili kuepuka magonjwa sugu ya figo ambayo matibabu yake yana ghrama kubwa sana.
Akizungumzia ugonjwa wa figo Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Figo MNH-Mloganzila Dkt. Immaculate Goima amesema watu wenye changamoto za magonjwa ya kisukari na shinikizo la juu la damu wanapaswa kutumia dawa kulingana na ushauri wa wataalam wa afya ili kutoathiri figo zao.
“Magonjwa yasiyoambukiza hususani figo yanaweza kuzuilika, ndio maana tunatoa rai kwa jamii kuepuka mambo yote yanayoweza kusababisha magonjwa haya kwakuwa matibabu yake ni gharama sana ukilinganisha na vipato vyetu na pia yanaathiri uzalishaji katika jamii kwakuwa mtu akipata maradhi haya atatumia muda mwingi kuhangaikia matibabu” ameongeza Dkt. Goima.
Aidha, Dkt. Goima amesisitiza jamii kubadili mtindo wa maisha kwa kuzingatia mlo na kufuata ushauri unaotolewa na wataalam wa lishe sambamba na kufanya mazoezi mara kwa mara ili kuendelea kujikinga magonjwa yasiyoambukiza husani magonjwa ya figo.
Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani inakadiriwa kuwa asilimia 10 ya watu duniani wana ugonjwa sugu wa figo na kwa Hospitali ya Taifa Muhimbili-Mloganzila katika kliniki yake ya magonjwa ya figo ambayo hufanywa mara mbili kwa wiki huona wagonjwa 20 hadi 30 ambapo pia wagonjwa wanaopata huduma ya kuchuja damu katika hospitali hiyo ni takribani 90.






