OMAN YAIPA TANZANIA VIFAA VYA KISASA VYA TEHAMA KUIMARISHA ULINZI WA TAARIFA ZA SERIKALI
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Ridhiwani Kikwete (kulia), akipokea sehemu ya vifaa vya kisasa vya kuimarisha mfumo wa kanzidata za TEHAMA kutoka kwa Balozi wa Oman nchini, Said Hilal Al Shidhan, wakati wa hafla ya makabidhiano iliyofanyika jijini Dodoma mapema wiki hii. (Picha na Rajabu Shariff).
DODOMA: Serikali ya Tanzania imepokea msaada wa vifaa vya kisasa vya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) kutoka Serikali ya Oman, hatua inayotarajiwa kuimarisha mfumo wa kanzidata, usimamizi wa kumbukumbu na ulinzi wa taarifa za Serikali.
Akipokea vifaa hivyo, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Ridhiwani Kikwete, alisema msaada huo utachangia kuongeza usalama wa taarifa za Serikali na kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi kupitia mifumo ya kidijitali.
Alisema mfumo huo utawezesha upatikanaji wa nyaraka kwa haraka, kuimarisha usimamizi wa kumbukumbu za Serikali na kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma kwa umma.
"Mfumo huu wa kidijitali utaboresha TEHAMA, utaongeza upatikanaji wa nyaraka kwa wakati na kuboresha huduma kwa umma," alisema Ridhiwani.
Katika hafla hiyo, ujumbe wa Tanzania uliongozwa na Waziri Ridhiwani Kikwete, huku upande wa Oman ukiongozwa na Balozi wa Oman nchini, Said Hilal Al Shidhan. Ujumbe wa Tanzania pia ulihusisha Balozi Abdallah Kilima pamoja na maafisa waandamizi kutoka pande zote mbili.
Kwa upande wake, Balozi Said Hilal Al Shidhan alisema msaada huo ni sehemu ya jitihada za kuendeleza uhusiano wa kihistoria na ushirikiano uliopo kati ya Tanzania na Oman katika sekta mbalimbali za maendeleo.
Alisema Serikali ya Oman itaendelea kushirikiana na Tanzania katika maeneo yenye manufaa ya pamoja kwa lengo la kuimarisha maendeleo na uhusiano wa kidiplomasia kati ya mataifa hayo mawili.




