RAIS SAMIA: UZINDUZI WA SAFARI ZA TRENI YA KISASA YA SGR NI MAANA HALISI YA KAZI IENDELEE
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, leo Agosti 1, 2024, ameandika historia katika kufanya mapinduzi makubwa ya usafiri nchini ambapo amezindua rasmi safari za treni ya kisasa ya umeme ya SGR, ya kwanza Afrika Mashariki.
Mhe. Dkt. Samia amefanya uzinduzi huo kuanzia stesheni 0 ya Tanzaniate jijini Dar Es Salaam, kisha kusimama kwa muda stesheni ya Pugu, kwa ajili ya kuwasalimia wananchi, kisha kuendelea na safari kuelekea Morogoro, ambapo kabla ya kufika Morogoro alisimama kwa muda stesheni ya Ngerengere na kusalimia wananchi.
Safari iliendelea hadi Dodoma, ambako ndiko alifanya uzinduzi rasmi wa safari hizo na kuzungumza na wananchi.
Uzindjuzi huo ulishuhudiwa na viongozi wakuu wa serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, wakiwemo mawaziri.
Viongozi hao ni pamoja na Makamu wa Rais, Mhe. Dkt. Philip Mpango, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi, Waziri Mkuu, Mhe. Kassim Majaliwa, Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Doto Biteko, Spika wa Bunge Mhe. Dkt. Tulia Ackson.
Wengine ni pamoja na Rais mstaafu, Mhe. Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, Makamu wa Rais Mstaafu, Mhe. Dkt. Mohammed Gharib Bilal na Rais Mstaafu wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Mhe. Dkt. Aman Abeid Karume na viongozi wa vyama vya siasa.
Akihutubia hadhara iliyohudhuria hafla hiyo, alisema, “Uzinduzi wa safari hizo ndio maana halisi ya Kazi Iendelee. Miradi yote ya kimkakati iliyoachwa na mtangulizi wangu Hayati Dkt. John Pombe Magufuli inakamilika kwa viwango bora, mradi wa SGR sio ndoto tena bali ni uhalisia, hakika kazi inaendelea.” Alisema Mhe. Dkt. Samia.
Alisema gharama za mradi mzima hadi utakapokamilika ni Dola za Marekani bilioni 10 sawa na shilingi Trilioni 23.3.
Mhe. Dkt. Samia pia alisema, “Reli imeongeza ari na hamasa na imekuwa chachu kwa watanzania kuamua kwamba hatma ya nchi yetu ni sisi wenyewe. Matarjio ni kwamba reli imeanzisha ushoroba wa shughuli za maendelea kote itakakopita.” Alisema.
“Tunaposema tunaifungua nchi, basi tunaifungua nchi Kavu Majini na Angani.”
Hakikisheni ujenzi wa vipande vilivyosalia unakamilika kwa wakati na kwa viwango vinavyokubalika, hakikisheni ujenzi wa meli nao unakamilika, lakini pia kuingiza reli kwenye Terminal III ya Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) na kuingia kwenye reli.
Akitoa maelezo ya mradi huo, Waziri wa Uchukuzi, Profesa Makame Mnyaa Mbarawa amesema, uzinduzi huo ni wa vipande viwili vyenye urefu wa Kilomita 722 kutoka Dar Es Salaam hadi Dodoma, ambao umegharimu kiasi cha shilingi trilioni 10.2, kati ya hizo trilioni 6.89 sawa na asilimia 68% ya fedha iloyotumika hadi sasa zimetolewa na serikali.
“Vipande vitano (5) vipya vyenye urefu wa KM 1,560 kati ya 2,102 ya ujenzi wa reli yote ya SGR unaendelea, Reli hii ndiyo itakuwa reli ndefu zaidi yenye kutumia umemem barani Afrika.” Amesema Profesa Mbarawa.
Aidha, kipande cha saba ambacho ni Uvinza- Msongati hadi Gitega nchini Burundi na kisha Kindu nchini DRC, kiko mbioni kuanza.
Katika hatua nyingine Mhe. Dkt. Samia alitangaza majina ya stesheni hizo kama ifuatavyo.
Dar Es Salaam, itaitwa Stesheni ya Magufuli, Morogoro itaitwa Stesheni ya Jakaya Kikwete, Dodoma itaitwa Stesheni ya Samia Suluhu Hassan, Tabora itaitwa Stesheni ya Ali Hassan Mwinyi, Shinyanga itaitwa Stesheni ya Abeid Aman Karume na Kigoma itaitwa Stesheni ya Mkapa
Source K-VIS BLOG



















