Breaking News

IDADI YA MAOMBI YA WANAFUNZI WA SAYANSI (YST) 2025 YAVUNJA REKODI

Dar es salaam - Mwanzilishi Mwenza wa Shirikisho la Wanasayansi Chipukizi (YST) Dokta Gozibert Kamugisha amesema kwa mwaka 2025 Shirikisho hilo limepokea idadi kubwa ya maombi ya kazi za kisayansi kutoka kwa wanafunzi wanaomba kushiriki mashindano hayo.

Kauli hiyo ameitoa mapema leo April 27, 2025 jijini Dar es Salaam wakati akizungumzia maandalizi ya maonyesho ya mwaka huu ambayo yatafanyika Septemba 18, 2025 Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), amesema mpaka kufika mwezi machi 2025 wamepokea jumla ya maombi ya kazi za kisayansi 1,516 .
Dk. Kamugisha amesema maombi hayo ni ambayo ni ongezeko la asilimia 43 ikilinganishwa na maombi 1,055 ya kazi za kisayansi yaliyowasilishwa mwaka mwaka 2024.

"Jumla wanafunzi 3,032 wameshiriki kutuma maombi idadi hii inatokana na kila ombi moja la kazi ya sayansi linawasilishwa kwa ushirikiano wa wanafunzi wawili". Alisema Dkt. Kamugisha.

Amesema kwa mwaka huu kumekuwepo na mwitiko mkubwa ya maombi ya kisayansi ikilinganishwa na miaka ya nyuma ni matokeo ya jitihada na mipango imara ya program za mafunzo ya kisayansi shuleni inayoendeshwa na YST katika mikoa yote nchini.
Dkt. Kamugisha aliongeza kwa mwaka huu 2025 jumla ya wanafunzi 6,064 na walimu wa sayansi 402 walishiriki katika mpango huo wa mafunzo ya kisayansi shuleni kisha kuchaguliwa kazi za sayansi 360 zitakazoendelea kupatiwa mafunzo katika duru ya pili.

"Yote haya yanafanyika kwa lengo ni kuhakikisha kuwa kazi za Kisayansi zitakazoonyesha katika mashindano ya YST 2025 zinakuwa na viwango na ubora unaoridhisha". Alisema Dkt. Kamugusha 

Aidha Dkt. Kamugisha aliongeza kuwa kazi zote za kisayansi ambazo wanafunzi wanaendelea kuzifanyia utafiti kwa sasa zimejikita katika kutafiti njia za kutatua changamoto mbalimbali za maendeleo.
Akielezea sababu za mashindano ya mwaka huu kufanyikia UDSM Dkt. Kamugisha amesema lengo ni kuwaleta pamoja katika jukwaa moja wanasayansi chipukizi kutoka shule za sekondari na wanasayansi wabobevu kutoka chuo hicho kikuu na vingine ili kupata ushauri juu ya namna bora ya kuboresha gunduzi zao.

“Kupitia Mpango wa kuibua na kulea vipaji vya kisayansi kwa vijana ambao unadhaminiwa na Karimjee Foundation (KFI) Tunaamini kupitia mpango huu vijana ambao ni wanasayansi chipukizi wataendelea kuhamasika zaidi katika kufanya gunduzi mbalimbali za kisayansi.” Alisema Dkt. Kamugisha

Kwa upande wake Ofisa wa Masoko Karimjee Foundation, Cobus van Zyl amesema tangu mwaka 2012 tumekuwa wadhamini Wakuu wa YST na kila mwaka wamekuwa wakitoa ufadhili wa masomo ya elimu ya juu kwa wanafunzi ambao wameshinda katika kundi la washindi wa jumla na kundi maalumu la elimu katika mashindano hayo.
Aliongeza kuwa ufadhili huu hauishii tu kwenye elimu bali unalenga kuboresha maisha ya kijana wa kitanzania ambapo hadi sasa wahitimu 49 wa YST wamepokea ufadhili wa masomo kutoka Karimjee Foundation.

“Mafanikio haya ni fahari kubwa kwetu kuanzia katika taaluma za uhandisi na sayansi ya Afya hadi uhifadhi wa mazingira na sera. Ushirikiano huu ni mfano wa jitihada wa uwajibikaji wa Karimjee Foundation na YST ambao kwa pamoja unaonesha dhamira ya kukuza elimu nchini hususani sayansi na teknolojia kwa vijana". Alisema Van Zyl.