Breaking News

RAIS WA NAMIBIA AWASILI TANZANIA KWA ZIARA RASMI YA SIKU MBILI

Rais wa Jamhuri ya Namibia, Mheshimiwa Dkt. Netumbo Nandi-Ndaitwah, amewasili nchini Tanzania leo, Mei 20, 2025 kwa ziara rasmi ya siku mbili inayotarajiwa kuhitimishwa Mei 21, 2025.

Ziara hii ni ya kwanza kwa Mheshimiwa Nandi-Ndaitwah tangu aingie madarakani mwezi Machi mwaka huu, na inafanyika kufuatia mwaliko rasmi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Mara baada ya kuwasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere jijini Dar es Salaam, Rais Nandi-Ndaitwah alipokelewa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mheshimiwa Balozi Mahmoud Thabit Kombo.
Katika ziara yake, Rais Nandi-Ndaitwah atafanya mazungumzo ya faragha na mwenyeji wake, Rais Samia Suluhu Hassan, yatakayofuatiwa na mazungumzo rasmi ya kuimarisha ushirikiano kati ya Tanzania na Namibia.

Aidha, viongozi hao wanatarajiwa kuzungumza na waandishi wa habari kuhusiana na makubaliano yatakayofikiwa katika mazungumzo yao, kabla ya kushiriki dhifa ya kitaifa ya chakula cha jioni iliyoandaliwa na Rais Samia kwa heshima ya mgeni wake.
Kesho Mei 21, Rais Nandi-Ndaitwah atatoa mhadhara maalum katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, kisha kutembelea Kituo cha Urithi wa Ukombozi wa Afrika kilichopo jijini Dar es Salaam.

Tanzania na Namibia zinaendelea kudumisha ushirikiano wa kihistoria ulioasisiwa na waasisi wa mataifa haya mawili – Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na Hayati Sam Nujoma – kupitia mikataba ya ushirikiano wa pande mbili na ndani ya Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC).