Breaking News

WAZALISHAJI WA NONDO SASA KUZALISHA KWA VIWANGO SAHIHI - WMA

Dodoma – Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Vipimo (WMA), Bw. Alban Kihulla, ameeleza kuwa kwa sasa wazalishaji wa nondo nchini wameanza kuzalisha bidhaa hizo kwa kuzingatia viwango sahihi vya urefu na unene.

Akitoa taarifa ya utendaji kazi wa WMA kwa Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Dkt. Selemani Jafo, alipokutana na menejimenti ya Wakala hiyo jijini Dodoma, Bw. Kihulla alisema hatua hiyo ni mafanikio makubwa katika kulinda maslahi ya walaji.

“Mhe. Waziri, ni habari njema kwamba sasa hivi wazalishaji wa nondo wanazalisha katika urefu ambao umekamilika na unene ambao uko sahihi. Sasa hivi walaji wetu wanapata bidhaa hiyo katika urefu na unene ulio sahihi,” alisema Kihulla.

Aidha, alibainisha kuwa mafanikio hayo yametokana na usimamizi thabiti wa WMA pamoja na ushirikiano mzuri kati ya Serikali na wadau wa sekta ya viwanda.