CUF YAITAKA SERIKALI ITUMIE BUSARA KUMALIZA MGOGORO NA KANISA LA UFUNGUO NA UZIMA
Dar es Salaam, Juni 30, 2025 — Chama cha CUF – Chama Cha Wananchi kimeitaka Serikali kuchukua hatua za haraka na kutumia busara katika kushughulikia mvutano unaoendelea kati ya Dola na Kanisa la Ufufuo na Uzima linaloongozwa na Askofu Josephat Gwajima, ili kuepusha machafuko na madhara kwa wananchi.
Kupitia taarifa iliyotolewa na Mkurugenzi wa Habari, Uenezi na Mahusiano na Umma wa chama hicho, Eng. Mohamed Ngulangwa, CUF kimesema kinasikitishwa na jinsi hali ilivyofikia na kuonya kwamba ikiwa busara haitatumika, kuna uwezekano wa kutokea maafa makubwa.
“CUF – Chama Cha Wananchi kinaamini kwamba busara ina nafasi kubwa ya kumaliza sintofahamu hii, na kwamba njia ya suluhu ni bora zaidi kuliko kutunishiana misuli,” ilieleza taarifa hiyo.
Chama hicho kimetoa kumbukumbu ya matukio ya nyuma kama sakata la bucha ya nguruwe la Mbokomu, Manzese mwaka 1993/94 na vurugu zilizotokea wakati wa kufungwa kwa Msikiti wa Mwembechai mwaka 1998 ambapo watu kadhaa walipoteza maisha, kikieleza kuwa hali ya sasa ina mwelekeo wa kurudia makosa ya kihistoria ikiwa tahadhari haitachukuliwa.
CUF imeonya kuwa namna serikali itakavyoshughulikia suala hili inaweza kuwa na athari kubwa kitaifa na kimataifa, na hivyo kuitaka ichukue hatua kwa hekima na maridhiano.
“Tunatoa wito kwa Serikali kulimaliza sakata hili kwa njia ya suluhu kabla madhara makubwa hayajatokea na kuongeza dosari mbele ya jicho la Jumuiya za Kimataifa,” amesema Eng. Ngulangwa.
CUF imesisitiza kuwa haki, usawa na amani kwa wote ni msingi muhimu wa jamii na hivyo ni wajibu wa kila upande kuhakikisha migogoro kama hii haigeuki kuwa ya kijamii au ya kidini.




