DKT. DOTO MASHAKA BITEKO ACHUKUA FOMU JIMBO LA BUKOMBE
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Mashaka Biteko, ambaye pia ni Mbunge anayemaliza muda wake wa Jimbo la Bukombe, ameanza rasmi safari ya kutetea nafasi yake ya Ubunge kwa kuchukua na kurejesha fomu ya kugombea kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Dkt. Biteko alichukua na kurejesha fomu hiyo leo Juni 29, 2025, kwa Katibu wa CCM Wilaya ya Bukombe, Ndugu Leonard Yesaya Mwakalukwa, katika ofisi za chama hicho wilayani humo.
Zoezi la uchukuaji na urejeshaji wa fomu za kugombea nafasi mbalimbali za uongozi ndani ya CCM linaendelea nchi nzima, ambapo wanachama mbalimbali wameendelea kujitokeza kuwania nafasi za Ubunge na Udiwani kuelekea Uchaguzi Mkuu ujao.
Dkt. Biteko amekuwa Mbunge wa Bukombe kwa vipindi mfululizo na anatajwa kuwa miongoni mwa viongozi wenye ushawishi mkubwa ndani ya serikali na chama.







