MADELEKA NA NTOBI WATEULIWA BARAZA KIVULI LA ACT WAZALENDO
Dar es Salaam — Chama cha ACT Wazalendo kimetangaza mabadiliko mapya katika Baraza Kivuli la Mawaziri, likiwajumuisha sura mpya na kuwahamisha baadhi ya viongozi wake ili kuimarisha usimamizi wa Serikali kwa niaba ya wananchi.
Kiongozi wa chama hicho, Ndugu Dorothy Manka Semu, alitangaza uteuzi huo leo jijini Dar es Salaam, huku akieleza kuwa mabadiliko hayo yamefanyika kwa mashauriano na Waziri Mkuu Kivuli, na yanalenga kuongeza ufanisi katika kusimamia sekta mbalimbali, hasa wakati ambapo Bunge linaongozwa na wabunge wa chama tawala.
Taarifa rasmi iliyotolewa na Katibu Mkuu Kiongozi wa chama, Ndg. Idrisa Kweweta, inaeleza kuwa uteuzi huo umezingatia weledi na uzoefu wa viongozi walioteuliwa. Miongoni mwa walioteuliwa ni:
Ndg. Mbarala Maharagande, aliyekuwa Waziri Kivuli wa Katiba na Sheria, sasa ni Waziri Kivuli wa Nishati.
Ndg. Peter Madeleka, mwanasiasa aliyejiunga na ACT Wazalendo kutoka CHADEMA, sasa ni Waziri Kivuli wa Katiba na Sheria.
Ndg. Thomas Sagwa Nkola ameteuliwa kuwa Naibu Waziri Kivuli wa Mifugo na Maendeleo ya Uvuvi.
Ndg. Emmanuel Reuben Ntobi, ambaye pia ni mhamiaji kutoka CHADEMA, ameteuliwa kuwa Naibu Waziri Kivuli wa Habari, Mawasiliano na TEHAMA.
Kwa mujibu wa Ndg. Abdallah Khamis, Afisa wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa ACT Wazalendo, mabadiliko haya ni sehemu ya juhudi za chama hicho katika kuhakikisha kuwa masuala ya kitaifa yanapata ufuatiliaji na uwajibikaji wa kutosha, licha ya mazingira magumu ya kisiasa ndani ya Bunge.
“Chama kimejipanga kuhakikisha kuwa sauti ya wananchi inasikika na masuala ya umma yanapewa uzito unaostahili,” alisema Khamis.
Mabadiliko haya yanakuja wakati ambao ACT Wazalendo inaendelea kujidhihirisha kama sauti mbadala ndani ya medani ya siasa za upinzani nchini Tanzania.





