Breaking News

SHEKHE PONDA AANZA NA CCM, AITAKA IJIANDAE KUONDOKA MADARAKANI, AWATAKA WATANZANIA KUCHAGUA ACT WAZALENDO

# Awahamasisha wananchi kushiriki uchaguzi mkuu na kuiangusha CCM Oktoba mwaka huu

Dar es Salaam - Katibu wa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu Tanzania ambaye pia ni mwanasiasa mkongwe, Shekhe Ponda Issa Ponda, ameendelea kuonesha msimamo wake dhidi ya Chama cha Mapinduzi (CCM) kwa kuitaja serikali yake kuwa imeshindwa kuwaletea maendeleo Watanzania, na hivyo kuwaomba wananchi kukiunga mkono Chama cha ACT Wazalendo katika uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba mwaka huu.

Akihutubia maelfu ya wananchi katika mkutano wa hadhara uliofanyika leo katika viwanja vya Mwembe Yanga, Temeke, jijini Dar es Salaam, Shekhe Ponda ambaye hivi karibuni alijiunga rasmi na ACT Wazalendo, alisema kuwa CCM haina jipya la kuwasaidia Watanzania na imeishiwa sera na dira ya maendeleo.
“Ndugu zangu wananchi, nimesimama hapa nikiwa na kofia mbili, kiongozi wa dini na mwanasiasa. Tayari nimechukua kadi ya ACT Wazalendo ili niwe na sifa ya kisheria ya kuwatetea Watanzania waliopoteza matumaini yao kwa muda mrefu. Serikali ya CCM imeshindwa kabisa kudhibiti vitendo vya utekaji, umasikini umeongezeka, huduma hospitalini ni ghali, hata maiti zinadaiwa. Hii sio Serikali ya watu,” alisema Shekhe Ponda huku akishangiliwa na umati wa watu.

Akiendelea kuzungumza, aliongeza: “CCM imekuwa madarakani kwa zaidi ya miaka 50, lakini hali ya maisha inazidi kuwa mbaya. Mwaka huu tunapaswa kufanya mabadiliko ya kweli kwa kuichagua ACT Wazalendo ili tuweze kuleta mawazo mapya ya maendeleo kwa Taifa letu.”
Katika mkutano huo, Mgombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia ACT Wazalendo, Dorothy Semu, naye aliwahamasisha wananchi kushiriki kikamilifu katika uchaguzi na kuitumia fursa hiyo kuiondoa CCM madarakani kwa kuwa, kwa mujibu wake, imeshindwa kutatua matatizo ya msingi ya wananchi.

“Tumeona vijana wahitimu wa vyuo vya ualimu wakiendelea kuhangaika mitaani. Serikali inadai walimu wapo wa kutosha wakati mahitaji ni zaidi ya walimu 270,000, lakini waliopo mitaani ni zaidi ya 140,000. Hali hiyo imejikita pia katika sekta ya afya na kilimo. CCM imegeuza afya ya Mtanzania kuwa bidhaa ya kifurushi. Tunahitaji serikali inayojali maisha ya watu, siyo biashara ya huduma za msingi,” alisema Semu.
Kwa upande wake, Makamu Mwenyekiti wa ACT Wazalendo, Isihaka Mchinjita, alisema kuwa ni wajibu wa wananchi kuhakikisha kuwa mwaka huu wanatumia kura zao kuiondoa CCM, ambayo amesema imeshindwa kabisa kutimiza majukumu yake ya msingi.

“Kama Serikali itaheshimu kura, wananchi watumie kura kuiondoa. Lakini kama Serikali itatumia vibaka kuiba kura, basi wananchi wasikubali kuibiwa. Hatuwezi kuendelea kuwa na Serikali ya namna hii, tuitumie Oktoba hii kama fursa ya ukombozi wa kweli wa Taifa letu,” alisema Mchinjita.
Kwa upande wake, Makamu Mwenyekiti wa ACT Wazalendo, Isihaka Mchinjita, alisema kuwa ni wajibu wa wananchi kuhakikisha kuwa mwaka huu wanatumia kura zao kuiondoa CCM, ambayo amesema imeshindwa kabisa kutimiza majukumu yake ya msingi.

“Kama Serikali itaheshimu kura, wananchi watumie kura kuiondoa. Lakini kama Serikali itatumia vibaka kuiba kura, basi wananchi wasikubali kuibiwa. Hatuwezi kuendelea kuwa na Serikali ya namna hii, tuitumie Oktoba hii kama fursa ya ukombozi wa kweli wa Taifa letu,” alisema Mchinjita.
Akihitimisha mkutano huo, Katibu Mkuu wa ACT Wazalendo, Ado Shaibu, alisema kuwa mchakato wa kumtambulisha Shekhe Ponda hautaishia Temeke tu, bali utaendelea katika maeneo mengine ya Dar es Salaam ikiwemo Ubungo, Kinondoni, Mbagala, Chamazi na majimbo yote ya mkoa huo. Alitoa wito kwa wananchi kujitokeza kwa wingi katika mikutano hiyo ya hadhara.

Mkutano huo wa Mwembe Yanga umeonekana kuwa mwanzo wa kampeni kali za upinzani kuelekea uchaguzi mkuu wa Oktoba 2025, huku Shekhe Ponda akionekana kuwa mmoja wa sauti mpya zenye mvuto kwa wananchi katika mchakato huo wa mabadiliko.