ACT WAZALENDO: JESHI LA POLISI ACHENI KUINGILIA MCHAKATO WA UCHAGUZI
Dar es Salaam – Chama cha ACT Wazalendo kimetoa tamko kali kikilaani hatua ya Jeshi la Polisi na baadhi ya Wakuu wa Wilaya kuanza kuwasiliana na viongozi wa chama hicho kuwataka wawasilishe majina ya watia nia wa Ubunge na Udiwani.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na chama hicho, maeneo yaliyoripotiwa kuhusika na mawasiliano hayo yasiyo ya kisheria ni pamoja na Kilwa, Kigamboni, Kinondoni, Magu na Tarime. Chama hicho kimeeleza kuwa hakuna msingi wa kisheria unaolazimisha chama cha siasa kuwasilisha taarifa za wagombea kwa Jeshi la Polisi au Wakuu wa Wilaya.
ACT Wazalendo imesema kuwa hatua hiyo ni kinyume na sheria za uchaguzi na inalenga kuwatisha au kuwadhoofisha wagombea wake. “Hatua hii ya Jeshi la Polisi haina nia njema kwenye mchakato wa uchaguzi,” imesema taarifa ya chama hicho.
Hatua Zilizochukuliwa:
1. Barua kwa IGP: ACT Wazalendo imemuandikia Mkuu wa Jeshi la Polisi, Inspekta Jenerali Camilius Wambura, kutaka kusitisha mara moja zoezi hilo ambalo wamelitaja kuwa ni haramu.
2. Malalamiko kwa Msajili wa Vyama: Chama hicho kimewasilisha malalamiko kwa Msajili wa Vyama vya Siasa na kutaka hatua zichukuliwe dhidi ya vitendo vya Jeshi la Polisi na Wakuu wa Wilaya.
3. Maagizo kwa Viongozi wa Chama: Viongozi wa ACT Wazalendo nchini kote wameagizwa kutotoa taarifa zozote kuhusu wagombea kwa Jeshi la Polisi.
4. Barua kwa Tume ya Uchaguzi: ACT Wazalendo imeiandikia Tume ya Uchaguzi (INEC) kuitaka kutoa tamko rasmi dhidi ya uingiliaji huo wa Polisi kwenye mchakato wa uteuzi wa ndani wa vyama.
Wito wa ACT Wazalendo:
Jeshi la Polisi litakiwe kusitisha mara moja zoezi hilo lisilo halali la kuwasiliana na viongozi wa chama kuhusu majina ya wagombea.
Viongozi wa chama waendelee kutotii maelekezo ya Jeshi la Polisi yanayokwenda kinyume na sheria.
ACT Wazalendo imesisitiza dhamira yake ya kushiriki Uchaguzi Mkuu wa 2025 kwa ujasiri, ikiahidi kupambana kwa ajili ya mageuzi hadi dakika ya mwisho.
Chama hicho kimeahidi kuendelea kuzikumbusha na kuzishinikiza mamlaka husika kuhakikisha uchaguzi huru, wa haki na wa kuaminika unafanyika – bila hofu wala upendeleo.




