Breaking News

CCM INAJALI UONGOZI WA VIJANA – JESSICA MSHAMA

Dar es Salaam – Katibu wa Idara ya Uhamasishaji na Chipukizi wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) Taifa, Ndg. Jessica Mshama, amesema kuwa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kinathamini sana mchango wa vijana katika uongozi, hali inayojidhihirisha kupitia kupewa kwao nafasi mbalimbali za juu za kiuongozi.

Akizungumza katika mahojiano na watangazaji wa kipindi cha Sentro kinachorushwa na Clouds TV, Ndg. Jessica alisema tofauti na vyama vingine, CCM imekuwa na uthabiti wa kiuongozi kwa kuwaamini vijana na kuwajengea mazingira ya kushiriki kikamilifu katika maamuzi ya kisiasa na kiuongozi.

"Ushindi wa CCM hautokani na bahati mbaya, bali ni matokeo ya msingi imara tuliojenga kwa vijana," alisema Ndg. Jessica, akisisitiza kwamba vijana ndio mhimili mkubwa wa mafanikio ya chama hicho.

Kuhusu maandalizi ya uchaguzi mkuu wa 2025, Ndg. Jessica alieleza kuwa UVCCM imekuwa ikiratibu mikutano na ziara mbalimbali katika mikoa tofauti nchini kwa lengo la kuhamasisha vijana kujitokeza kugombea nafasi mbalimbali za uongozi, sambamba na kujisajili na kujiandaa kupiga kura ifikapo Oktoba 2025.

Mahojiano hayo yalifanyika jana, tarehe 08 Julai 2025, katika studio za Clouds TV, jijini Dar es Salaam.