GCLA YAWAKARIBISHA WANANCHI KUJIFUNZA MASUALA YA KEMIKALI KATIKA MAONESHO YA SABASABA
Dar es salaam - Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali (GCLA) imewataka wananchi kujitokeza kutembelea banda lao katika Maonesho ya 49 ya Biashara ya Kimataifa ya Sabasaba (DITF), ili kupata elimu kuhusu masuala mbalimbali yanayohusu kemikali.
Wito huo umetolewa na Mkurugenzi wa Huduma za Uchunguzi wa Mazingira wa GCLA, Dkt. Peter Shimo, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari katika maonesho hayo yanayoendelea jijini Dar es Salaam.
Dkt. Shimo amesema lengo kuu la mamlaka hiyo ni kuhakikisha jamii inapata uelewa sahihi kuhusu kemikali na shughuli nyingine zinazofanywa na GCLA, hususan katika usimamizi salama wa matumizi ya kemikali nchini.
“Hapa tunatoa huduma mbalimbali ikiwemo usajili wa kemikali, utoaji wa elimu kwa wananchi kuhusu shughuli zetu, pamoja na kusajili wajasiriamali wanaojihusisha na kemikali,” amesema Dkt. Shimo.
Aidha, amewataka wajasiriamali wanaojihusisha na matumizi au biashara ya kemikali kutembelea banda hilo ili kupata elimu sahihi na kufanya usajili wa shughuli zao, ikiwa bado hawajafanya hivyo.
“Wajasiriamali wanaofika hapa ambao wanajishughulisha na shughuli za kemikali bila kuwa na usajili, watapewa maelekezo ya kina kuhusu taratibu za kufuata ili kukamilisha usajili huo,” ameongeza.
Dkt. Shimo pia amebainisha kuwa GCLA ina mfumo wa usajili wa mtandaoni kwa ajili ya kuwafikia wajasiriamali walioko mbali na huduma za moja kwa moja, hatua inayolenga kurahisisha upatikanaji wa huduma kwa wananchi wote.
Maonesho ya 49 ya Biashara ya Kimataifa ya Sabasaba yanaendelea katika viwanja vya Mwalimu Nyerere, barabara ya Kilwa jijini Dar es Salaam.




