INEC YAWATAKA WASIMAMIZI WA UCHAGUZI KUSOMA KATIBA NA SHERIA ILI KUIMARISHA UCHAGUZI HURU NA HAKI
Dar es salaam - Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) imewataka waratibu wa uchaguzi wa mikoa, wasimamizi wa uchaguzi, wasimamizi wasaidizi wa ngazi ya jimbo, pamoja na maofisa ununuzi, kutenga muda wao kusoma Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, sheria za uchaguzi na maelezo mbalimbali yanayotolewa na Tume hiyo.
Lengo la wito huo ni kuwawezesha viongozi hao kusimamia uchaguzi mkuu kwa ufanisi, kwa mujibu wa sheria, ili kuhakikisha uchaguzi unakuwa huru, haki na unaozingatia misingi ya demokrasia.
Kauli hiyo imetolewa na Balozi Omar Ramadhan Mapuri, mjumbe wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, wakati wa ufunguzi wa mafunzo ya siku tatu kwa wasimamizi wa uchaguzi wapatao 108 kutoka halmashauri za Bagamoyo, Mkuranga, Rufiji, Chalinze pamoja na maeneo ya mikoa ya Dar es Salaam na Pwani.
Balozi Mapuri alisema mafunzo hayo yanatolewa kwa lengo la kuwaongezea maarifa na uzoefu wasimamizi hao katika kipindi chote cha uchaguzi mkuu, sambamba na kuzingatia sheria, kanuni na miongozo ya uchaguzi.
“Sheria na miongozo ya uchaguzi inawataka wasimamizi kuhakikisha kuwa mchakato wa upigaji kura unafanyika kwa haki, uwazi na kwa kuzingatia ushiriki wa wananchi wote walioko katika maeneo yao ya kiutawala, ikiwa ni pamoja na kata na mikoa,” alisema.
Aidha, aliipongeza NEC kwa kusimamia na kuratibu uendeshaji wa chaguzi nchini kwa mujibu wa sheria, jambo ambalo linalenga kulinda demokrasia kwa manufaa ya wananchi, vyama vya siasa pamoja na wagombea wa nafasi mbalimbali.
Tume ya uchaguzi imeeleza kuwa itaendelea kutoa mafunzo na miongozo ya mara kwa mara kwa wahusika wa uchaguzi, ili kuhakikisha kuwa uchaguzi wa mwaka huu unafanyika kwa ufanisi, haki na kwa kuzingatia misingi ya utawala bora.













