Breaking News

RAIS WA TAFF AREJEA NCHINI, ATAJA MIKAKATI KUKUZA TASNIA YA FILAMU AFRIKA MASHARIKI

Na Neema Mpaka, Dar es Salaam – Rais wa Shirikisho la Filamu Tanzania (TAFF), Rajabu Amiry, ameshiriki mkutano wa siku tatu uliofanyika Kampala, Uganda, uliowakutanisha Marais na viongozi wa mashirikisho ya vyama vya watayarishaji wa filamu ("filmmakers") kutoka nchi nane za Afrika.

Akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kurejea nchini, Rajabu Amiry amesema kuwa mkutano huo umefanikiwa kwa kiasi kikubwa, ambapo viongozi hao wamesaini makubaliano ya ushirikiano (MOU) yatakayochangia kukuza tasnia ya filamu pamoja na kufungua milango ya masoko ya kazi za wasanii wa filamu katika ukanda huo.

“Tumeweza kukutana na Marais wa mashirikisho mengine ya filamu, tukabadilishana uzoefu na kujadili mikakati ya pamoja ya kuinua tasnia ya filamu. Hii ni fursa kubwa kwa waigizaji na watayarishaji wa filamu nchini, hivyo wajiandae kwa mambo mazuri yanayokuja,” alisema Amiry.

Ameishukuru serikali ya Uganda kwa udhamini wa mkutano huo, na pia kuipongeza UNESCO kwa kufadhili na kuiamini Tanzania pamoja na Zanzibar kushiriki katika tukio hilo muhimu kwa maendeleo ya sekta ya filamu barani Afrika.
Kwa upande wake, Afisa Filamu Ally Makata alisema kuwa Bodi ya Filamu Tanzania inaendelea kuweka mikakati thabiti ya kuhakikisha tasnia ya filamu pamoja na michezo ya kuigiza nchini inapata maendeleo endelevu.

“Malengo yetu ni kuhakikisha filamu za Kitanzania zinafikia viwango vya kimataifa, na ushiriki katika mikutano kama hii unatoa nafasi kwa wasanii wetu kupata maarifa mapya na ushirikiano wa kimataifa,” alisema Makata.

Mkutano huo unatarajiwa kuwa chachu ya mageuzi katika tasnia ya filamu Afrika, hasa kwa nchi washiriki ambazo zimeonesha dhamira ya dhati ya kushirikiana kwa maendeleo ya pamoja.