RC CHALAMILA AWATAKA VIONGOZI WA DINI KUHUBIRI AMANI, UMOJA NA MSHIKAMANO KUELEKEA UCHAGUZI MKUU
Dar es Salaam, Tanzania – Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Mhe. Albert Chalamila, ametoa wito kwa viongozi wa dini kuendelea kuliombea Taifa amani na kuhubiri ujumbe wa utulivu hususan katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi mkuu.
Akizungumza leo jijini Dar es Salaam katika kikao maalum na viongozi wa dini, Mhe. Chalamila amesema kuwa viongozi wa dini ni nguzo muhimu katika kulinda amani ya nchi. Amesisitiza kuwa serikali kupitia Jeshi la Polisi itaendelea kuimarisha ulinzi, huku akiwataka Watanzania kujifunza kutokana na madhara ya uvunjifu wa amani yanayoshuhudiwa katika baadhi ya mataifa jirani.
"Hakuna kiongozi anayetaka kuona wananchi wake wakikumbwa na machafuko au vitendo vya ukatili. Ni wajibu wa kila mmoja wetu, hususan viongozi wa dini, kuhakikisha wanatumia nafasi walizonazo kuhubiri na kuhimiza amani kupitia madhabahu na nyumba za ibada," alisema Mhe. Chalamila.
Kwa upande wake, Sheikh wa Mkoa wa Dar es Salaam ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Amani ya Mkoa huo, Sheikh Walid Kawambwa, alieleza kuwa viongozi wa dini wana nafasi kubwa ya kujenga maadili na kuimarisha mshikamano katika jamii. Alisisitiza kuwa wataendelea kushirikiana na wadau mbalimbali kuhakikisha nchi inaendelea kubaki katika hali ya amani.
Naye Mtume Boniface Mwamposa wa makanisa ya Arise and Shine, alihimiza viongozi wa dini kutumia vyema madhabahu katika kueneza ujumbe wa amani, upendo, na mshikamano miongoni mwa Watanzania
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Mhe. Edward Mpogolo, alikiri mchango mkubwa wa viongozi wa dini katika kuombea amani na kuhimiza utulivu wa taifa, akibainisha kuwa wamekuwa wakishirikiana kwa karibu na makundi mbalimbali katika jamii, yakiwemo ya wafanyabiashara na waendesha bodaboda, katika kuhakikisha jamii inaendelea kuwa salama.
Kikao hicho kilihitimishwa kwa viongozi wa dini kuahidi kuendelea kuwa mabalozi wa amani na mshikamano katika kipindi chote cha kuelekea uchaguzi mkuu na hata baada ya uchaguzi.











