Breaking News

TPDC KIDEDEA MAONESHO YA 49 YA SABASABA, YAJINYAKULIA TUZO YA MAZINGIRA

Dar es salaam - Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano katika Shirika la Maendeleo ya Petroli na Gesi Tanzania (TPDC), Bi. Maria Mselemu, amesema utendaji bora wa shirika hilo umechangia ushindi wao kwenye Maonesho ya 49 ya Biashara ya Kimataifa maarufu kama Sabasaba.

Akizungumza mara baada ya kukabidhiwa tuzo hiyo, Bi. Mselemu amesema TPDC imekuwa ikifanya vizuri katika maeneo mbalimbali, jambo lililosababisha kushinda tuzo tano tofauti katika historia ya maonesho hayo, ikiwemo tuzo ya mazingira waliyotunukiwa mwaka huu.

“Kwetu hii ni tuzo ya tano kwenye maonesho haya, lakini kwa TPDC hii siyo jambo la kushangaza kwani tumekuwa tukipata tuzo mbalimbali, ikiwemo ya mazingira kutokana na jitihada zetu za kulinda mazingira kupitia matumizi ya nishati safi,” alisema Mselemu.
Akifafanua kuhusu tuzo hiyo ya mazingira, Bi. Mselemu alieleza kuwa matumizi ya nishati safi ya kupikia na kwenye magari yamesaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza uchafuzi wa hewa.

“Tumefanikwa kuondoa tani zaidi ya laki moja za hewa ukaa kwa kutumia nishati safi. Ubunifu na umakini katika utekelezaji wa miradi yetu ni sababu kubwa ya mafanikio haya,” aliongeza.

TPDC imeendelea kuonesha mfano wa taasisi ya umma inayotekeleza majukumu yake kwa ufanisi huku ikichangia kwa kiasi kikubwa katika ulinzi wa mazingira na maendeleo endelevu ya nishati nchini.