ACT MGUU SAWA KUELEKEA UCHAGUZI MKUU 2025, WATUMA SALAMU CCM
Dar es Salaam – Chama cha ACT-Wazalendo kimesema kimejipanga kwa umakini mkubwa kuhakikisha kinakiondoa madarakani Chama cha Mapinduzi (CCM) katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025, kwa njia ya kidemokrasia.
Akizungumza leo wakati wa Mkutano Mkuu Maalum wa chama hicho unaoendelea katika Ukumbi wa Mlimani City, jijini Dar es Salaam, Katibu Mkuu wa ACT-Wazalendo, Ado Shaibu, amesema chama hicho kimejifunza kutokana na historia ya mfumo wa vyama vingi tangu miaka ya 1990 hadi sasa, na kimeweka mkazo mkubwa katika mipango ya kimkakati kwa ajili ya ushindi.
"Tangu uchaguzi wa mwaka 2020, ACT Wazalendo imekuwa ikitathmini mambo yaliyofanywa vyema na wapinzani, sambamba na kufanyia kazi maeneo ya udhaifu ambayo kwa muda mrefu yamekuwa kikwazo kwa upinzani," alisema Ado.
Aliongeza kuwa chama hicho sasa kina "silaha za kutosha" za kisiasa, kimaadili na kimkakati, kuhakikisha mabadiliko ya kweli ya kiuongozi yanapatikana kupitia sanduku la kura.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa ACT-Wazalendo, Othman Masoud Othman, ambaye pia ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, alisisitiza kuwa Mkutano huo si wa kawaida, bali ni hatua muhimu ya kurejesha mamlaka kwa wananchi.
“Mkutano huu unakwenda kutengeneza ramani ya kuwapatia Watanzania sauti zao, ambazo zimekabwa, zimenyimwa na zimezuiwa kwa muda mrefu,” alisema Othman.
Amesema mkutano huo haukulenga kupanga miundombinu ya uchaguzi wala kutafuta kura, bali ni wa kuandaa mwelekeo mpya wa kisera utakaowapa wananchi nafasi ya kweli ya kushiriki katika maamuzi ya taifa lao.
“Binadamu yeyote aliyenyimwa sauti hizi mbili – ya kumuweka kiongozi na ya kumwajibisha – anaishi utumwani, hata kama anaishi katika kasri lenye raha,” aliongeza Othman huku akiwaonya viongozi na wajumbe wa mkutano huo dhidi ya kuwasaliti wananchi kwa kukosa maono ya mabadiliko.
Naye Kiongozi wa chama hicho, Dorothy Semu, amesema uamuzi wa chama kushiriki uchaguzi huo umetokana na dhamira ya dhati ya kuleta mabadiliko ya kweli kwa Watanzania.
“Hatukuchagua kushiriki uchaguzi kwa sababu ya mapenzi, bali kwa sababu ya dhamira dhamira ya kulinda haki ya kuchagua, dhamira ya kurejesha thamani ya kura,” alisema Semu.
Alisisitiza kuwa historia imeonesha kuwa kususia uchaguzi hakujawahi kuleta mabadiliko, na kwamba ACT-Wazalendo iko tayari kwa mapambano ya kidemokrasia ili kuondoa CCM madarakani.
“Serikali ya CCM imeshindwa kusimamia ipasavyo uchumi, huduma za jamii, na masuala ya utawala bora. Watanzania wengi wanaishi katika umaskini, bila ajira, wakikosa huduma bora, na wakiwa hawana sauti,” alisema Semu.
Alimalizia kwa kusema: “Tumeingia vitani na tutatoka na ushindi!”











