Breaking News

CHAMA CHA NLD CHAZINDUA ILANI YA UCHAGUZI MKUU 2025

Katibu Mkuu wa NLD, Doyo Hassan Doyo wa kwanza kulia, Katibu wa Kamati ya Uandaaji wa Ilani, Fahadi Hassan Doyo (katikati) akiongea katika hafla ya Uzinduzi wa ilani ya chama hicho, makao makuu ya chama jijini dar es salaam 
Katibu wa Kamati ya Uandaaji wa Ilani, bwana Fahadi Hassan Doyo akifafanua jambo kwa waandishi wa habari katika hafla ya Uzinduzi wa ilani ya chama cha NLD, makao makuu ya chama hicho jijini dar es salaam 

Dar es Salaam – Chama cha National League for Democracy (NLD) kimezindua rasmi Ilani yake ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025, ikiwa ni hatua muhimu kuelekea uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika mwezi Oktoba mwaka huu.

Ilani hiyo imewasilishwa kwa umma na uongozi wa chama ikiwa ni dira ya kisera kwa mgombea urais wa NLD, Mhe. Doyo Hassan Doyo, anayewania nafasi ya kuongoza Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kipindi cha miaka mitano ijayo.

Ikiwa imejengwa juu ya misingi ya Uzalendo, Haki na Maendeleo, Ilani ya NLD imeainisha vipaumbele vinne vikuu vinavyolenga kuleta mabadiliko ya kweli na maendeleo jumuishi kwa Watanzania wote.

Ajira kwa Wote
Katika kukabiliana na changamoto ya ukosefu wa ajira, hasa kwa vijana, NLD inapendekeza kuanzisha viwanda vidogo na vya kati, kuendeleza kilimo cha kisasa, na kuwezesha wanawake na vijana kupitia mikopo, mafunzo na ujasiriamali.

Elimu Bora na Jumuishi
Chama kinatilia mkazo elimu bora inayopatikana kwa wote bila ubaguzi. Kipaumbele kitatolewa katika kuboresha mazingira ya kujifunzia na kufundishia pamoja na maslahi ya walimu.

Afya kwa Maendeleo ya Taifa
Ilani inalenga kuboresha huduma za afya kwa kuimarisha upatikanaji wa dawa, vifaa tiba, miundombinu ya afya, na kupanua huduma za bima ya afya kwa wananchi wote, wakiwemo wa kipato cha chini.

Miundombinu ya Kukuza Uchumi
NLD imeahidi kuwekeza katika barabara, reli, nishati, na teknolojia ya mawasiliano kwa lengo la kuimarisha uchumi, kupunguza gharama za uzalishaji na kuongeza ushindani wa taifa katika soko la kikanda na kimataifa.

Kupitia Ilani hii, NLD inaeleza dhamira yake ya kuleta mabadiliko ya kweli yanayowalenga watu, uchumi wa taifa, na ustawi wa jamii kwa ujumla.

Chama hicho kimewataka Watanzania kuungana na kuunga mkono mwelekeo mpya wa taifa kwa kumpa Mhe. Doyo Hassan Doyo ridhaa ya kuwaongoza, ili kujenga Tanzania yenye Uzalendo, Haki na Maendeleo.