MAMLAKA YA HIFADHI YA ENEO LA NGORONGORO (NCAA) YASHIRIKI MAONESHO YA NANE NANE 2025
Arusha, Dodoma, Mbeya - Mamlaka ya Hifadhi ya Eneo la Ngorongoro (NCAA) inashiriki kikamilifu katika Maonesho ya Wakulima ya Nane Nane kwa Kanda ya Kaskazini, Kati na Nyanda za Juu Kusini yanayofanyika katika viwanja vya Themi Njiro - Arusha, Nzuguni - Dodoma na John Mwakangale - Mbeya.
Kupitia ushiriki wake, NCAA inatoa elimu kwa wananchi kuhusu vivutio vya utalii vinavyopatikana ndani ya Hifadhi ya Ngorongoro, urithi wa utamaduni na mambo kale, uhifadhi shirikishi, maendeleo ya jamii pamoja na fursa mbalimbali za uwekezaji zinazopatikana ndani ya hifadhi hiyo maarufu barani Afrika.
Wananchi wanahimizwa kutembelea mabanda ya NCAA ili kujifunza mengi kuhusu Hifadhi ya Ngorongoro, ambayo ni kivutio namba moja cha utalii barani Afrika na mojawapo ya maeneo yanayopendwa zaidi na wageni wa safari kwa mujibu wa tovuti ya TripAdvisor.
Maonesho ya Nane Nane ya mwaka huu yalianza rasmi tarehe 1 Agosti 2025 na yanatarajiwa kufikia tamati tarehe 8 Agosti 2025. Kaulimbiu ya mwaka huu ni: “Chagua Viongozi Bora kwa Maendeleo Endelevu ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi 2025.”
NCAA inaendelea kuwakaribisha Watanzania na wageni wote kutembelea mabanda yake ili kupata maarifa na kufahamu mchango wake katika uhifadhi, utalii, na maendeleo ya jamii nchini.







