Breaking News

MAONESHO YA MASHARIKI CREATIVE ECONOMY EXPO 2025 KUFANYIKA AGOST 14 JIJINI DAR

Dar es Salaam – Taasisi ya Culture and Development East Africa (CDEA) kwa kushirikiana na Tamasha la Tuzo za Filamu pamoja na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, imeandaa Maonesho ya Mashariki Creative Economy Expo 2025 yatakayofanyika kuanzia Agosti 14 hadi 16 mwaka huu katika Ukumbi wa Mlimani City, Dar es Salaam.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi wa CDEA, Bi. Ayeta Wangusa amesema maonesho hayo yatakutanisha wadau mbalimbali wa sekta ya ubunifu wakiwemo wajasiriamali, watunga sera, wawekezaji pamoja na wabunifu kutoka Afrika Mashariki na maeneo mengine.

“Maonesho haya ya siku tatu yatafunguliwa kuanzia saa tatu asubuhi hadi saa kumi na mbili jioni. Kutakuwa na soko la kazi za ubunifu ikiwemo mitindo, ufundi, uchapishaji na filamu, sambamba na midahalo, mafunzo na burudani, vyote vikilenga kukuza uchumi jumuishi na endelevu wa ubunifu,” alisema Bi. Ayeta.

Kwa mujibu wa Ayeta, siku ya pili kutakuwa na mazungumzo kuhusu uchumi wa muziki, mafunzo ya ubunifu katika nyanja za muziki, filamu, mitindo, uandishi, uzinduzi wa ripoti ya UNESCO kuhusu tasnia ya vitabu Afrika, kikao cha uelewa kuhusu COSOTA pamoja na usiku wa onesho maalum ‘Usiku wa Shot’ utakaofanyika katika Nafasi Art Space.

Siku ya mwisho ya maonesho hayo itahusisha mjadala kuhusu sera za filamu ambapo Tanzania itatumia mwongozo wa Afrika Mashariki kutokana na ukosefu wa sera ya kitaifa ya filamu. Aidha, kutakuwa na muendelezo wa mafunzo ya ubunifu, onesho la mitindo (fashion show) pamoja na vyumba maalum kwa ajili ya wafanyabiashara wa sekta ya filamu kubadilishana uzoefu.
Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi Msaidizi wa Sanaa za Ufundi kutoka Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA), Bi. Bona Masenge amesema kuwa wamepokea mradi huo kwa furaha kubwa, akisisitiza kuwa utasaidia wabunifu kujitangaza katika Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Aidha, amesema tayari kamati maalum ya kitaifa inayohusisha wadau mbalimbali imeanza vikao kuhakikisha maandalizi yote yanakamilika kwa wakati, huku akiwataka wasanii na wadau kujisajili mapema ili kushiriki maonesho hayo.

Naye Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo kutoka Bodi ya Filamu, Bw. Emmanuel Ndumukwa amesema kuwa maonesho haya ni fursa adhimu kwa wasanii kujifunza na kubadilishana uzoefu, pamoja na kujua namna bora ya kutumia mitandao ya kijamii kwa tija ya kiuchumi.

CDEA ni taasisi ya maarifa na kituo cha fikra za ubunifu kilichopo Dar es Salaam, kinachojihusisha na kukuza sekta ya ubunifu kupitia utafiti, uvumbuzi na majukwaa ya kuwawezesha wasanii na wajasiriamali wa ubunifu kutoka Afrika Mashariki.