WAJUMBE CUF WAZICHAPA KATIKA MKUTANO WA KUTEUA WAGOMBEA URAIS
Dar es Salaam Kikao cha Baraza Kuu la Uongozi wa Chama cha Wananchi (CUF) kilichotarajiwa kujadili na kupitisha Ilani ya Uchaguzi pamoja na majina ya wagombea wa urais upande wa Tanzania Bara na Zanzibar kilianza kwa taharuki baada ya kuzuka kwa vurugu ukumbini.
Video iliyosambaa mitandaoni inaonesha baadhi ya wajumbe wa chama hicho wakizozana na kushikana mashati muda mfupi kabla ya kikao kuanza rasmi. Vurugu hizo zinasemekana kuibuka baada ya kuwasili kwa baadhi ya viongozi waandamizi wa chama, ambapo kulikuwa na madai ya kuwepo kwa wajumbe wasio halali waliodaiwa kuingizwa ukumbini kimakosa.
Akizungumza baada ya tukio hilo, Mkurugenzi wa Mawasiliano kwa Umma wa CUF, Mohamed Ngulangwa, alithibitisha kutokea kwa hali hiyo na kueleza kuwa baadhi ya wajumbe walikuwa na nia ya kuvuruga kikao hicho muhimu. Hata hivyo, alibainisha kuwa walinzi walifanikiwa kudhibiti hali hiyo na kikao kiliendelea kama kilivyopangwa.
Kulikuwa na watu waliolenga kuvuruga kikao, lakini hatua za haraka zilichukuliwa kuhakikisha usalama na utulivu unarejea. Kikao kimeendelea salama na ajenda zilizopangwa zinatekelezwa kama kawaida," alisema Ngulangwa.
Mkutano huo una umuhimu mkubwa kwa CUF kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025, kwani unahusisha uteuzi wa wagombea wa nafasi ya juu ya uongozi pamoja na kupitisha Ilani ya chama itakayotumika katika kampeni.
Hadi sasa, taarifa rasmi kuhusu majina ya wagombea wa urais yatakayopitishwa bado hazijatolewa, huku macho na masikio ya wanachama na wananchi yakiwa yamelenga matokeo ya kikao hicho.



