WANAFUNZI WA SHULE YA MSINGI BROTHER MARTIN DODOMA WAPATA ELIMU KUHUSU VIPIMO
Dodoma - Wanafunzi wa Shule ya Msingi Brother Martin kutoka mkoani Dodoma wamepata elimu kuhusu masuala ya vipimo kutoka kwa Meneja Mawasiliano na Uhusiano kwa Umma wa Wakala wa Vipimo (WMA), Bi. Veronica Simba, katika banda la Wakala huo lililopo kwenye Maonesho ya Nanenane yanayoendelea katika Viwanja vya Nanenane Nzuguni jijini Dodoma.
Akizungumza na wanafunzi hao, Bi. Simba alieleza kuwa WMA imeweka mikakati mbalimbali ya kupanua wigo wa utoaji elimu ya vipimo, ikiwemo kuanzisha vilabu vya vipimo katika shule mbalimbali nchini. Lengo la mpango huo ni kuwajengea wanafunzi uelewa wa kina kuhusu umuhimu wa matumizi sahihi ya vipimo katika maisha ya kila siku na kuchochea nidhamu ya matumizi ya vipimo sahihi katika biashara na shughuli nyingine za kijamii.
Maonesho ya Nanenane hutoa fursa kwa taasisi mbalimbali kutoa elimu kwa umma kuhusu huduma wanazotoa, ambapo Wakala wa Vipimo ni miongoni mwa taasisi zinazotumia maonesho haya kufikisha ujumbe kuhusu umuhimu wa vipimo sahihi kwa maendeleo ya kiuchumi na kijamii.






