WANAFUNZI WANUFAIKA NA ELIMU YA VIPIMO KATIKA MAONYESHO YA NANENANE
Dodoma — Wanafunzi kutoka shule mbalimbali wamepata fursa ya kuelimishwa kuhusu masuala ya vipimo walipotembelea banda la Wakala wa Vipimo (WMA) katika siku ya nne ya Maonesho ya Kilimo ya Nanenane yanayoendelea katika Uwanja wa Nzuguni, jijini Dodoma.
Kupitia maonesho hayo, WMA imetoa elimu ya kina kuhusu matumizi sahihi ya vipimo na umuhimu wake katika shughuli za kila siku, hususan katika biashara na huduma. Lengo ni kuongeza uelewa wa jamii kuhusu haki katika vipimo, ili kuimarisha usawa na uadilifu kwenye mizani na vipimo mbalimbali.
Katika hatua nyingine, WMA imetangaza mkakati wa kuanzisha vilabu vya elimu ya vipimo katika shule mbalimbali nchini. Mpango huo unalenga kupanua wigo wa utoaji elimu hiyo kwa wanafunzi na jamii kwa ujumla, ili kuijenga Tanzania yenye haki katika vipimo.
Maonesho ya Nanenane huandaliwa kila mwaka kwa lengo la kuhamasisha maendeleo ya kilimo na kuwapa wananchi fursa ya kujifunza teknolojia na huduma mbalimbali zinazohusiana na sekta ya kilimo na biashara.






