Breaking News

WAZALISHAJI MAUDHUI MTANDAONI WAONYWA KUEPUKA TAARIFA ZA UCHOCHEZI KUELEKEA UCHAGUZI MKUU 2025

Dar es Salaam, Agosti 3, 2025 – Wazalishaji wa maudhui mtandaoni wametakiwa kuzingatia maadili na kuepuka kusambaza taarifa za uchochezi, uvumi, au lugha za chuki ambazo zinaweza kusababisha taharuki na machafuko nchini, hasa katika kipindi hiki cha kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani unaotarajiwa kufanyika baadaye mwaka huu.

Wito huo umetolewa na Meneja wa Kitengo cha Huduma za Utangazaji kutoka Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), Injinia Andrew Kisaka, wakati akiwasilisha mada katika mkutano ulioandaliwa na Tume Huru ya Uchaguzi (INEC) kwa ajili ya watoa maudhui mtandaoni.

Injinia Kisaka amesema kuwa kipindi cha uchaguzi huwa na mazingira ya migawanyiko, mivutano ya kijamii, na upotoshaji wa hali ya juu, hivyo ni wajibu wa mabloga na watoa maudhui mtandaoni kuwa makini na kuchukua hatua za kulinda amani ya nchi.

“Ni muhimu mabloga waepuke kusambaza uvumi, waripoti kwa umakini, wasipendelee upande wowote na wakemee lugha za chuki. Kama unaona maudhui yanaweza kusababisha taharuki, ni bora usiyachapishe kabisa,” amesema Kisaka.

Ametoa mfano wa historia ya machafuko ya uchaguzi yaliyotokea katika nchi za Nigeria (2011) na Kenya (2007), ambako zaidi ya watu 1,000 walipoteza maisha na maelfu kufurushwa makwao kutokana na taarifa za uchochezi na upotoshaji ulioenezwa kupitia vyombo vya habari na mitandao.

Katika mazingira haya, amesema Kisaka, vyombo vya habari vinaweza kuchangia ama kupunguza machafuko kulingana na jinsi vinavyotoa taarifa. Ametoa wito kwa vyombo hivyo kuhakikisha vinafuata miongozo ya kuripoti wakati wa uchaguzi ili kuzuia maafa.

“Uvumi ni chanzo kikuu cha vurugu. Vyombo vya habari vinapaswa kuchunguza kwa kina kabla ya kuchapisha taarifa, na kutoa taarifa sahihi haraka iwezekanavyo ili kuzuia mzunguko wa taarifa potofu na za kisasi,” amesema.

Aidha, amewahimiza mabloga kutoandika vichwa vya habari vya kichochezi au kurudia kauli za uchochezi kutoka kwa wanasiasa, hata kama zinaonekana kuvutia wasomaji. Amesisitiza kuwa lugha ya matusi au udhalilishaji inaweza kusababisha watu kuchukua hatua za kikatili.

Injinia Kisaka pia amewataka mabloga kuwa waangalifu wanapotoa matangazo ya moja kwa moja ya mikutano ya kampeni, akisisitiza kuwa kazi hiyo inapaswa kufanywa na waandishi waandamizi waliobobea, si kwa mtindo wa ‘one man show’.

“Matangazo ya moja kwa moja ya vurugu au machafuko yanapaswa kufanywa kwa weledi mkubwa. Wanaohamasisha chuki na vurugu hawapaswi kupewa jukwaa la kuzungumza kupitia majukwaa ya habari,” amesema.

Pia amesisitiza kuwa vyombo vya habari vinapaswa kuzuia kuonesha picha za machafuko ambazo zinaweza kuchochea hisia kali, na kwamba ni vyema kusitisha matangazo ya moja kwa moja iwapo hali itazidi kuwa mbaya.

Mkutano huo uliolenga kutoa elimu kwa mabloga umeelezwa kuwa ni sehemu ya mikakati ya kuhakikisha uchaguzi wa mwaka 2025 unafanyika kwa amani, huku wahusika wote wakitakiwa kushiriki katika kulinda amani ya taifa.