BRELA YATOA WITO KWA WAFANYABIASHARA KUJISAJILI
Kaimu Meneja wa Viwanda wa BRELA, Yusuph Nakapala akifafanua jambo wakati akiongea na waandishi wa habari katika Maonesho ya Nane ya Teknolojia ya Madini yanayoendelea mkoani Geita
Geita - Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) imewataka wafanyabiashara wakubwa, wadogo pamoja na kampuni kujitokeza kusajili majina ya biashara, alama za biashara na kuwasilisha mizania ya mwaka kwa mujibu wa sheria.
Wito huo ulitolewa na Kaimu Meneja wa Viwanda wa BRELA, Yusuph Nakapala, katika Maonesho ya Nane ya Teknolojia ya Madini yanayoendelea mkoani Geita.
“Mwanzoni mwitikio ulikuwa mdogo lakini sasa tunashukuru kuona wateja wanajitokeza kwa wingi. BRELA tupo tayari kuwasaidia kutatua changamoto zao, hivyo wajitokeze zaidi ili kutimiza matakwa ya kisheria,” alisema Nakapala.
Aliongeza kuwa mbali na usajili wa majina na alama za biashara, BRELA pia inatoa huduma za usajili wa hataza, utoaji wa leseni za biashara za kundi A, leseni za viwanda, vyeti vya usajili, uwasilishaji wa taarifa za maendeleo ya viwanda pamoja na taarifa za miliki za manufaa za kampuni.
Mfanyabiashara Kiliani Muyezi aliyepata huduma za usajili alisema huduma za BRELA ni za haraka na rafiki. “Ukikamilisha taratibu zote, unapata nyaraka zako papo hapo bila kusubiri. Nawaomba wafanyabiashara wenzangu wajitokeze ili kufanya biashara kwa uhuru na kwa mujibu wa sheria,” alisema Muyezi.
Kwa upande wake, mkazi wa Geita, Zedekia Gabriel alisema licha ya awali kukumbana na ucheleweshaji wa usajili wake, alipofika kwenye banda la BRELA tatizo lake liliweza kutatuliwa mara moja.









