DKT. ABBASI AFUNGUA MAFUNZO YA ELIMU YA UTALII WA ANGA KWA WADAU WA UTALII
Karatu, Arusha – Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Dkt. Hassan Abbasi, leo amefungua mafunzo ya siku tatu ya elimu ya utalii wa anga (astrotourism) yanayofanyika Karatu, mkoani Arusha.
Mafunzo hayo yameratibiwa na Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA) kwa kushirikiana na Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT), na yanaendeshwa na wataalamu kutoka Astrotourism Aotearoa (New Zealand), Smithsonian Astrophysical Observatory (Harvard, Marekani) pamoja na Dark Sky International yenye makao yake Arizona, Marekani.
Akifungua mafunzo hayo, Dkt. Abbasi alisema kuwa hatua hiyo ni sehemu ya mkakati wa wizara kufungua mazao mapya ya utalii, ikiwemo utalii wa anga. Alibainisha kuwa kupitia mafunzo hayo, Watanzania watapata maarifa na ujuzi kuhusu aina hiyo mpya ya utalii, vifaa vinavyotumika pamoja na fursa zilizopo.
Kwa upande wake, Naibu Makamu Mkuu wa OUT, Prof. Saganga Kapaya, alisema Tanzania imebarikiwa kuwa na fursa kubwa za kuendeleza utalii wa anga kwani zaidi ya theluthi moja ya ardhi yake imehifadhiwa, hivyo maeneo mengi yana anga lenye giza usiku. Aliongeza kuwa hali hiyo inaiwezesha Tanzania kuona anga kwa zaidi ya asilimia 95 ukilinganisha na nchi nyingine za Afrika.
Naye Prof. John Hearnshaw kutoka New Zealand, ambaye ni mwezeshaji wa mafunzo hayo, alieleza kuwa washiriki watafundishwa maeneo manne makuu: namna ya kuendesha utalii wa anga kwa kushirikisha jamii na wadau, elimu ya fizikia ya anga, matumizi ya telescope, pamoja na upigaji picha za anga.
Mafunzo hayo yamehudhuriwa na washiriki zaidi ya 70 wakiwemo wasafirishaji watalii, waongoza watalii, waendeshaji huduma za malazi, taasisi za serikali zinazohusika na utalii (TTB na ZCT), taasisi za uhifadhi (NCAA, TANAPA, TAWA, TFS), taasisi za elimu na utafiti (NCT, ACWM-Mweka, VETA, OUT), wataalamu na wasimamizi wa utalii, wanasayansi wa anga, wajasiriamali, pamoja na watunga sera.










